Urusi yapinga azimio la UN la kuzuia silaha za nyuklia
25 Aprili 2024Nchi 13 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ziliunga mkono azimio hilo huku Urusi ikitumia kura yake ya turufu dhidi ya azimio hilo na China haikupiga kura.
Baada ya kura hiyo, Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo Linda Thomas-Greenfield, alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin aliarifu kwamba nchi yake haina nia ya kupeleka silaha za nyuklia katika anga za mbali lakini hatua ya kupinga azimio hilo inaibua swali juu ya dhamira iliyojificha ya serikali ya nchi hiyo.
Azimio hilo lilikuwa linatoa wito kwa nchi zote kutotengeneza ama kupeleka silaha za nyuklia ama silaha nyingine za maangamizi makubwa angani, kama ilivyopigwa marufuku chini ya mkataba wa kimataifa wa 1967 uliozijumuisha Marekani na Urusi , na kukubaliana kuhusu hitaji la kuthibitisha utiifu.