1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema iko tayari kwa lolote vita vya Ukraine

6 Desemba 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema nchi yake iko tayari kuchukuwa hatua yoyote inayohitajika kuhakikisha kuwa mataifa ya Magharibi hayafanikishi kile yanachokiita "ushindi wa kimkakati".

https://p.dw.com/p/4nopo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.Picha: Khalil Hamra/AP Photo/picture alliance

Lavrov amesema uamuzi wa nchi yake kutumia makombora ya kisasa dhidi ya Ukraine ulidhamiria kuyafanya mataifa ya Magharibi yafahamu kwamba Moscow iko tayari kutumia njia yoyote inayowezekana kuhakikisha kuwa kamwe haitashindwa kimkakati.

Akizungumza  kwenye mahojiano na mwandishi wa habari Tucker Carlson wa Marekani hapo jana, Lavrov alisema ni kosa kubwa kwa mataifa ya Magharibi kudhani kwamba Urusi haina mipaka iliyowekwa ambayo haipaswi kuchupwa.

Soma zaidi: Marekani yasema Korea Kaskazini umetuma wanajeshi 10,000 Urusi

Wiki mbili zilizopita, Urusi ilitumia makombora yake mapya chapa Oreshnik dhidi ya mji wa Dnipro nchini Ukraine, baada ya mataifa ya Magharibi kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi.

Rais Vladimir Putin alisema makombora hayo yanasafiri kwa kasi iliyo mara kumi zaidi ya sauti na hayawezi kudunguliwa na mfumo wowote wa ulinzi.

Rais Volodymyr Zelensky aliyaita mashambulizi hayo kuwa kipimo cha juu kabisa cha wendawazimu wa Urusi, na alitowa wito wa nchi yake kupatiwa mifumo ya kisasa zaidi ya ulinzi ili kukabiliana na kitisho hicho.