Urusi yazidisha mashambulizi nchini Ukraine
13 Machi 2022Mapema leo makombora ya Urusi yaliishambulia kambi moja ya kijeshi magharibi mwa Ukraine karibu na mpaka wa Poland katika hujuma iliyosababisha vifo vya watu 35.
Kambi hiyo ya kijeshi imekuwa ikitumika pia na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuwapatia mafunzo wanajeshi wa Ukraine.
Pamoja na vifo vilivyotangazwa watu 134 pia wamejeruhiwa baada ya kiasi makombora 30 ya Urusi kuilenga kambi hiyo ya Yavoriv iliyopo karibu kilometa 25 kutoka mpaka wa Ukraine na Poland.
Shambulizi hilo limefanywa siku moja baada ya mwanadipomasia mmoja wa Urusi kuionya Marekani kama Moscow inaweza kuzilenga shehena za misaada ya kijeshi inayotumwa na mataifa ya magharibi kwenda Ukraine.
Kulengwa kwa kambi hiyo ya kijeshi kinafuatia mkururo wa mashambulizi yaliyofanywa na Urusi siku moja iliyopita yakiilenga miji kadhaa nchini Ukraine ikiwemo Mariupol na maeneo ya pembezoni mwa mji mkuu Kyiv.
Papa Francis atoa wito wa kusitishwa "mauaji ya kikatili"
Mapema Jumapili, kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis alikosoa vikali kile amekitaja kuwa "ukatili" kwa mauaji ya watoto na raia wa kawaida nchini Ukraine kutokana na vita inayoendelea.
Papa Francis ametoa wito wa kukomeshwa mashambulizi "kabla ya miji kugeuka kuwa makaburi"
"Kwa jina la Mwenyezi Mungu, ninawaomba: ´komesheni mauaji ya halaiki´'' amesema Papa Francis mbele ya umati wa karibu waumini 25,000 walikusanyika mbele ya viunga vya kanisa la mtakatifu Petro kuhudhuria ibada ya kila Jumapili.
Zelenskyy asema hakuna kusalimu amri mbele ya Urusi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameituhumu Urusi kwa kutengeneza "Jamhuri mpya bandia" kwa kuigawa Ukraine.
Amewataka Waukraine kutokubali maeneo zaidi kujetenga kama ilivyotokea kwa majimbo mawili ya mashariki yanayoegemea Urusi ambayo yalianza kupambana na vikosi vya serikali vya Ukraine mnamo mwaka 2014.
Katika wakati vikosi vya Urusi vinajitayarisha kuushambulia mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, rais Zelenskyy amesema ili Moscow iukamate mji huo itabidi pengine kwanza iuangamize kwa mabomu na kuwauwa wakaazi wake wote.
Mzozo baina ya mataifa hayo jirani ya Ulaya mashariki umeingia wiki ya tatu huku ukiwa umewalazimisha watu milioni 2.5 kutoka Ukraine kuikimbia nchini hiyo.