1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usafiri watatizika Kenya

Shisia Wasilwa/DW Nairobi12 Novemba 2018

Usafiri wa umma nchini Kenya umetatizika katika miji yote mikubwa baada ya kuanza kutekelezwa kwa sheria za barabarani.

https://p.dw.com/p/386kM
Nairobi Straßen Verkehr
Picha: AP

Usafiri wa umma nchini Kenya umetatizika katika miji yote mikubwa baada ya kuanza kutekelezwa kwa sheria za barabarani dhidi ya magari mabovu. Magari machache yaliyozingatia sheria hiyo yaliwatoza abiria nauli ya juu, huku mengine yakigoma kufuatia sheria hizo.

Hatua ya kuyaondoa magari ya abiria iliafikiwa jana jioni kwenye mkutano na chama cha wenye magari hayo. Serikali iliwapa muda wa majuma mawili wenye magari hayo kuzingatia sheria hizo lakini mengi ya magari hayajazingatia.

Wakenya wengi katika miji ya Nairobi, Mombasa, Nakuru, Kisumu na Eldoret, wamelazimika kutafuta njia mbadala ya usafiri. Baadhi walionekana wakitembea baada ya serikali kuanza kutekeleza sheria za barabarani maarufu, sheria za Michuki. Magari mengi ambayo hayana mikanda, vidhibiti mwendo pamoja na makanga na madereva wasio na sare rasmi yalikamatwa na kulemaza usafiri.

Sheria za 'Michuki'

Mabaki ya basi lililohusika katika ajali mwezi Oktoba Kericho-Kenya, na kusababisha vifo vya watu 51
Mabaki ya basi lililohusika katika ajali mwezi Oktoba Kericho-Kenya, na kusababisha vifo vya watu 51Picha: Getty Images/AFP/B. Ongoro

Sheria hizo ziliundwa miaka 15 iliyopitwa na aliyekuwa waziri wa barabara marehemu John Michuki kwa lengo la kuleta urazini kwenye sekta hiyo inayoendeshwa na wenye magari watundu. Hata hivyo watekelezaji wamezembea huku visa vya ajali vikiongezeka. John Kiplagat ni mmoja wa wasafiri. Kiplagat ameendelea kusema:

"Kuna interview nilikuwa niende Nairobi, nilikuwa nifike huko kwa masaa mawili, nilikuwa hapa saa kumi na mbili asubuhi, nahofia sasa sitaweza kufika huko, maanake nimezunguka stages zote za Nairobi sijapata gari lolote.”

Baadhi ya masuala ambayo vyama vya wenye matatu vinataka yamulikwe tena ni pamoja na matozo kwa wamiliki wa magari ya uchukuzi kwa kukiuka sheria za barabarani badala ya kutoza madereva na makanga wanaovunja sheria barabarani, kupaka magari yao rangi nyeupe na sare maalum zinazohitajika kwa madereva na makanga.

Wito kwa serikali na wadau wa matatu kuzungumza

Serikali imeagiza shirika la reli nchini kuongeza treni za kubeba abiria wakati huu operesheni
Serikali imeagiza shirika la reli nchini kuongeza treni za kubeba abiria wakati huu operesheniPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Kwa sasa wanatafuta kufanya mazungumzo na waziri wa uchukuzi. Samuel Mwangi ni mmoja wa madereva wa magari ya uchukuzi wa umma. Mwangi anaeleza kuwa:

"Ukinunua hizo vitu zote, ukienda inspection unaambiwa tena uende ukatekate, tunauliza wanaweza kutuonyesha mfano wa gari moja ambayo tunaweza kuifuata kama wenye matatu, sasa unakuta, ukiingia barabarani unatafutiwa makosa kidogokidogo.”

Wakati huo huo, Mamlaka ya Usafiri Salama wa Kitaifa imetangaza ada mpya za adhabu kwa wanaokiuka sheria za barabarani. Oktoba 25, serikali ilitangaza kuwa itaanza kutekeleza sheria za barabarani tarehe 12 mwezi huu. Samuel Kimaru ni kamanda wa Trafiki.

"Ile kitu ningewaomba, wacha sheria ifuatwe. Magari yaliyozingatia sheria, hatutakuwa na shida nayo, tumeanza leo na itaendelea, kama gari yako ni sawa hatuna maneno na wewe.” Amesema Kimaru.

Serikali imeagiza shirika la reli nchini kuongeza treni za kubeba abiria wakati huu operesheni ya kuyakamata magari mabovu inapoendelea. Aidha wenye magari wanaotoza nauli maradufu wameonywa kuwa watachukuliwa hatua kali za sheria. Takwimu zinaonyesha kuwa watu 2600 wameaga dunia tangu mwezi Januari mwaka huu kutokana na ukiukaji wa sheria za barabarani.


Mhariri: Mohammed Khelef