1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Usalama waimarishwa mjini New York

21 Machi 2023

Polisi mjini New York wameimarisha usalama kuelekea uwezekano wa kukamatwa kwa rais wa zamani Donald Trump kuhusiana na malipo aliyoyafanya kwa mwigizaji wa filamu za ngono.

https://p.dw.com/p/4P1Tt
USA | New York bereitet sich auf eine mögliche Festnahme von Trump vor
Picha: David Dee Delgado/REUTERS

Ili kumnyazisha asifichue aibu na siri zake, huku rais huyo wa zamani akitoa wito wa maandamano makubwa iwapo atashtakiwa. 

SOMA PIA; Trump anatarajia kukamatwa Jumanne

Ni wafuasi wachache tu wa Trump waliohudhuria maandamano katika mji mkuu wa kifedha wa Marekani Jumatatu jioni, wakati jopo kuu la wazee wa mahakama likizingatia uchunguzi wa Wakili wa Wilaya ya Manhattan Alvin Bragg juu ya malipo yaliyofanyika mwaka 2016 kwa muigizaji wa filamu za ngono Stormy Daniels.

Uchunguzi wa Bragg unahusu malipo ya dola 130,000 zilizolipwa wiki moja kabla ya uchaguzi wa 2016 ili kumzuia Daniels kutangaza hadharani kuhusu mahusiano yake ya wali na Trump.

Trump atoa wito wa maandamano

USA | Ex-Präsident Donald Trump bei der NCAA Wrestling Championships
Rais wa zamani wa Marekani Donald TrumpPicha: Sue Ogrock/AP/picture alliance

Trump atakuwa rais wa kwanza wa zamani au aliyeko madarakani kushtakiwa kwa uhalifu ikiwa mashtaka yatawasilishwa, hatua ambayo italeta mshtuko katika kinyang'anyiro cha 2024  ambapo Trump mwenye umri wa miaka 76 anagombea kurejea ofisini.

Bragg, mwanachama wa chama cha Demokratic hajathibitisha mipango yoyote hadharani, lakini amewasilisha mashahidi wakuu mbele ya mahakama katika wiki za hivi karibuni na kumpa Trump fursa ya kutoa ushahidi.

Mwishoni mwa juma Trump alisema kwamba anatarajia "kukamatwa" siku ya Jumanne na kuwataka wafuasi wake kuandamana na kile alichokiita "kurejesha taifa lao!" ingawa wakili wake alisema maoni hayo yalitokana na ripoti za vyombo vya habari na sio hatua zozote mpya za waendesha mashtaka.

SOMA PIA; Kamati ya Bunge la Marekani yatoa ripoti ya uvamizi wa Januari 6

Baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vilisema jopo hilo linaweza kupiga kura ya kufunguliwa mashitaka litakaporejea siku ya Jumatano baada ya kumhoji shahidi wake wa mwisho, wakili Robert Costello, siku ya Jumatatu.

Hatua zitakazochukuliwa

Idara ya polisi ya New york imejitayarisha kwa hatua isiyokuwa ya kawaida, ambayo itashuhudia kiongozi wa zamani wa Marekani akichukuliwa alama za vidole na ikiwezekana hata kufungwa pingu, kuweka vizuizi nje ya ofisi ya Bragg na nje ya ofisi ya Trump.

USA I Polizeidepartement (NYPD) am Times Square
Picha: Andrew Kelly/REUTERS

Wanachama wa chama cha Demokratic wameonya kwamba wito wa Trump unaweza kusababisha kurudiwa kwa ghasia ambazo wafuasi wake walianzisha kwenye makao makuu ya bunge la Marekani mnamo Januari 2021.

Katika kundi la mtandaoni linaloitwa "The Donald," baadhi ya wafuasi wa Trump walitoa wito wa "mgomo wa kitaifa" na "Vita vya wenyewe kwa wenyewe 2.0" ili kumlinda Trump na kupinga kukamatwa kwa mtu yeyote.

Lakini hakuna dalili ya vuguvugu kubwa kutoka kwa watu maarufu wanaomuunga mkono Trump, kama vile wanawe na watoa maoni wakuu kuhimiza waziwazi watu kuchukua hatua mitaani kama walivyofanya baada ya uchaguzi wa 2020, wakati Rais Joe Biden alipomshinda Trump.

 

//AFP, AP