1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushahidi zaidi wamuhusisha Trump na Urusi

8 Desemba 2018

Rais Donald Trump wa Marekani amekanusha kwamba uchunguzi wa waendesha mashitaka umepata ushahidi unaomuhusisha yeye na uingiliaji wa Urusi kwenye kampeni za uchaguzi wa urais wa 2016, ambao bilionea huyo alishinda.

https://p.dw.com/p/39jYT
G20-Gipfel in Buenos Aires | USMCA-Abkommen | Donald Trump, Präsident USA
Picha: Reuters/K. Lamarque

Akiandika kwenye mtandao wake wa Twitter siku moja baada ya waendesha mashitaka kueleza kwa undani jaribio lililokuwa halijulikani hapo awali la Urusi kusaidia kwenye kampeni hiyo, Trump amesema: "Baada ya miaka miwili na mamilioni ya kurasa (na gharama ya zaidi ya dola milioni 30), hakuna ushahidi!"

Siku ya Ijumaa (Desemba 7), ofisi ya mwendesha mashitaka maalum Robert Mueller na pia majalada ya mahakama ya New York yalianika ushahidi unaoonesha kuwa wakili wa zamani wa Trump, Michael Cohen, alikuwa na mawasiliano na Mrusi mmoja tangu mwaka 2015, ambaye alitoa pendekezo la "ushirikiano wa kisiasa" na timu ya kampeni ya Trump na pia akapendekeza mkutano kati ya mgombea huyo na Rais Vladimir Putin.

Ofisi hizo mbili kwa pamoja ziliweka hadharani mawasiliano yaliyokuwa hayakutajwa hapo kabla baina ya washirika wa Trump na wajumbe wa Urusi, ambayo yanaonesha kuwa Kremlin ilikusudia tangu mapema sana kuwa na ushawishi kwa Trump na timu yake ya kampeni kwa kutumia malengo yake ya kisiasa na maslahi yake ya kibiashara.

Ushahidi wamuweka pabaya Trump

USA Washington - Robert Mueller
Mchunguzi Maalum wa Marekani, Robert Mueller.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Kuwekwa hadharani kwa majalada ya kesi hizo, ambazo zinawahusisha Cohen na mwenyekiti wa zamani wa timu ya kampeni ya Trump, Paul Manafort, kunakuja kwenye wiki ambayo Mueller naye alikuwa anatoa matokeo ya uchunguzi wake uliokuwa ukiangalia uhusiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na ikulu ya Urusi, Kremlin.

Matokeo hayo yanaelekea kumgusa moja kwa moja Trump kwenye masuala kama ya mipango ya kulipa pesa kwa njia zisizo halali kisheria na pia kupingana na madai yake kwamba hakuwa na uhusiano wowote na Urusi.

Nyaraka za mahakama zinaonesha namna ambavyo mashahidi waliowahi kuwa washirika wa karibu sana wa Trump - kama Cohen ambaye aliwahi kusema kuwa yuko tayari kufa kwa ajili ya rais huyo - walivyotoa taarifa ambazo ni mbaya sana kumuhusu bilionea huyo katika jitihada zao za kujisafisha mbele ya serikali na kuwania kupunguziwa adhabu mahakamani.

Mshukiwa mmoja, mshauri wa zamani wa masuala ya usalama Michael Flynn, alitoa taarifa nyingi sana kwa waendesha mashitaka kiasi cha kwamba wiki hii Mueller alisema kwamba hakustahiki kufungwa tena jela.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo