1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Marekani: Biden ashinda jimbo la Michigan

5 Novemba 2020

Katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Marekani mgombea wa chama cha Democratik Joe Biden yumo njiani kufikia idadi ya kura za kumpeleka ikulu.

https://p.dw.com/p/3ktBB
US Wahlen 2020 | Präsidentschaftswahlen in den USA | Joe Biden
Picha: Carolyn Kaster/AP Photo/picture alliance

Matumaini sasa ni makubwa kwa Biden baada ya kulichukua jimbo la Michigan. 

Wakati huo huo rais Trump na timu yake wanataka kwenda mahakamani kupinga hesabu za kura. 

Mgombea urais wa chama cha Demokratik Joe Biden anakaribia kufikia idadi ya kura zinazohitajika kumfungulia mlango wa kuingia ikulu ya Marekani. Wakati idadi kamili inayohitajika ni kura 270 za wajumbe maalumu, Biden ameshatia kibindoni kura 264.

Hata hivyo mshindani wake rais Donald Trump amepinga hesabu hizo. Kambi ya kampeni ya Trump imesema imewasilisha malalamiko ya kisheria ili kusitisha kuhesabiwa kura za kwenye jimbo la Pennsylvania baada ya kutoa malalamiko juu ya hesabu za kura kwenye majimbo ya Michigan na Wisconsin.

Timu ya kampeni ya Trump inasema maafisa wa uchaguzi waliwazuia mawakala wao

US Wahl 2020 | Briefwahl Edgewater Colorado
Picha: Marc Piscotty/Getty Images

Waendesha kampeni wa kambi ya Trump wamewalaumu maafisa wa uchaguzi kwa kuwazuia mawakala wao kuzikaribia sehemu za kuhesabia kura kwenye jimbo la Pennsylvania. Mpaka sasa Trump amepata kura 214 za wajumbe wa baraza maalumu.

Matumaini ya Joe Biden ya kuingia Ikulu yalizidi kuwa makubwa baada ya kulichukua jimbo la Michigan lenye kura 16 za wajumbe maalumu. Joe Biden pia ameshinda kwenye jimbo lingine muhimu la Wisconsin.

Kutokana na matokeoya hadi sasa bwana Biden amesema anao uhakika wa kushinda uchaguzi na  ameeleza: "Rafiki zangu, ninao uhakika ,tutaibuka washindi lakini huu hautakuwa ushindi wa peke yangu.Huu utakuwa ushindi wa watu wa Marekani na ushindi wa demokrasia.Hapatakuwapo majimbo ya Republican na ya Democratik baada ya kushinda uchaguzi bali itakuwapo Marekani moja”.

Bwana Biden anaamini atakuwa mshindi baada ya kura kuhesabiwa. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 amesisitiza kwamba Marekani inapaswa kuondoa mgawanyiko mkubwa.

Wakati huo huo spika wa bunge la Marerakani Nanyc Pelosi amesema watu wa Marekani wameshaamua kwa njia ya kupiga kura na kwamba wanawapeleka Ikulu wagombea wao Joe Biden na Kamala Harris.

Pelosi amesema kwenye barua yake kwamba kuchaguliwa kwa Joe Biden itakuwa hatua ya kihistoria kutokana na kupigiwa kura na watu milioni 70, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya Marekani. Hata hivyo bibi Pelosi amesema chama cha Democratik kitakabiliwa na changamoto baada ya  kupoteza viti kadhaa bungeni.