Usitishaji mapigano jambo la lazima Gaza - UNRWA
31 Oktoba 2023Mkuu wa shirika hilo, Phillipe Lazzarini, ameuambia mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa kuwa usitishwaji mapigano kwa ajili ya kupisha shughuli za kibinaadamu limekuwa sasa suala la kufa na kupona kwa mamilioni ya watu katika Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: Netanyahu apuuza miito ya usitishwaji mapigano
Mkuu huyo wa UNRWA ameituhumu Israel kwa kile alichokiita kutoa "adhabu ya pamoja" dhidi ya Wapalestina na raia waliolazimika kuyahama makazi yao.
"Karibu asilimia 70 ya walioripotiwa kuuawa ni watoto na wanawake. Save the Children iliripoti jana kuwa karibu watoto 3,200 wameuawa Gaza katika wiki tatu tu. Hii inapindukia idadi ya watoto wanaouawa kila mwaka katika maeneo ya migogoro duniani tangu mwaka wa 2019." Alisema Lazzarini.
Soma zaidi: Maelfu ya watu wapora vituo vya misaada Gaza, yasema UN
Ameonya kuwa kuvunjika zaidi kwa utaratibu wa kiraia baada ya mabohari ya shirika hilo kuvamiwa na Wapalestina wanaotafuta chakula na misaada mingine kutafanya iwe vigumu sana kwa shirika hilo kubwa kabisa la Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza kuendelea kuhudumu.