1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji vita kati ya Israel na Hamas wacheleweshwa

23 Novemba 2023

Mpango wa kusitishwa mapigano kwa siku nne kati ya Israel na Hamas ili kuruhusu msaada kuingia Gaza na kuwachiwa mateka wanaoshikiliwa unatarajiwa kuanza kutekelezwa kwa mara ya kwanza baada ya karibu wiki saba za vita

https://p.dw.com/p/4ZKww
Mabomu yarindima katika Ukanda wa Gaza
Mapigano yanaendelea Gaza licha ya makubaliano ya kuweka chini silaha na kuwaachia matekaPicha: AFP

Hamas walisema mpango huo utaanza Alhamisi saa nne kamili asubuhi. Lakini Israel imesema mpango huo hautaanza hadi pengine kesho Ijumaa. Mshauri wa usalama wa taifa Tzachi Hanegbi amesema mawasiliano kuhusu kuwachiwa kwa mateka wao yanaendelea kupiga hatua. Aidha, Israel bado haijasema ni wakati gani itasitisha mashambulizi yake ya anga na ardhini katika eneo hilo la pwani.

Soma pia: Baraza la mawaziri la Israel laidhinisha makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka

Wakizungumza mjini Tel Aviv jana usiku katika kikao cha pamoja cha waandishi habari Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, waziri Benny Gantz na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, wameapa kuwaleta nyumbani mateka wote na kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas. Netanyahu amesema kuwa vita hivyo vitaendelea hadi watakapoyatimiza malengo yao.

Handaki lililopatikana chini ya hospitali ya Al-Shifa
Israel ilionyesha handaki la Hamas chini ya Al-ShifaPicha: Victor R. Caivano/AP/dpa/picture alliance

Netanyahu alisema shirika la Msalaba Mwekundu litaruhusiwa kuwatembelea mateka watakaobaki katika Ukanda Gaza akiongeza kuwa wakati mwingine kazi yake inahitaji maamuzi magumu.

Naye Waziri Gallant alisema ana matumaini ya dhati kuwa makubaliano ya kuwaachia mateka yatatekelezwa na matokeo ya mazungumzo yanayoendelea yataonekana katika siku chache zijazo.

Chini ya mpango huo, mateka 100 wataachiwa kutoka Gaza kwa kubadilishana na wafungwa 300 wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel. Aidha, malori yaliyobeba misaada ya dharura yataruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza ambako hakuna chakula, maji, umeme na dawa na vifaa vya matibabu.

Gaza mahali pabaya kabisa kwa watoto duniani – UNICEF

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF ameuita Ukanda wa Gaza uliozingirwa kuwa ni "sehemu hatari kabisa ya mtoto kuishi", na kusema kuwa makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas hayatoshi kuyaokoa maisha yao.

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

Soma pia: Umoja wa Mataifa umesifu makubaliano kati ya Israel na Hamas ya kuwaachilia mateka na kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Catherine Russell ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa zaidi ya watoto 5,000 wameripotiwa kuuawa huko Gaza tangu shambulizi la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, hiyo ikiwa ni asilimia 40 ya vifo mpaka sasa.

Russell amesema ili watoto waishi na wafanyakazi wa kibinaadamu wabaki eneo hilo na kufanya kazi yao kwa ufanisi, mipango ya kusitisha vita kwa nyakati fulani ili kuruhusu huduma za kiutu haijitoshelezi.

Uingereza yajadili kuwachiwa kwa mateka wote

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Uingereza David Cameron amejadiliana mjini London na viongozi wa nchi za Kiarabu na zenye Waislamu walio wengi kuhusu suluhisho la kisiasa kuelelekea kuwachiwa huru mateka wote. Taarifa ya serikali ya Uingereza imesema wanadiplomasia hao waliangazia jinsi ya kusaidia kuachiwa mateka wote, kuongeza msaada Gaza, na kufikia suluhisho la muda mrefu la kisiasa la mzozo huo.

Mawaziri wa Mambo ya Kigeni kutoka Saudi Arabia, Jordan, Misri, Mamlaka ya Palestina, Uturuki, Indonesia na Nigeria Pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kirabu na Balozi wa Qatar, walihudhuria mkutano huo.

afp, ap, reuters, dpa