1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Nitailemaza kiuchumi Uturuki ikiwashambulia YPG

14 Januari 2019

Uturuki imeapa kuendelea kupambana na wanamgambo wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani na ambao inawachukulia kama magaidi, baada ya Rais Donald Trump kuonya atauharibu vibaya uchumi wa Uturuki.

https://p.dw.com/p/3BV7D
USA, Texas, McAllen: Präsident Trump spricht mit Grenzpatrouillen während des Besuchs der US-Mexiko-Grenze
Picha: Reuters/L. Millis

Trump amesema atauharibu uchumi huo iwapo Uturuki itawashambulia wanamgambo hao wakati ambapo Marekani inaviondoa vikosi vyake nchini Syria.

Msemaji wa Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan Ibrahim Kalin aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba hakuna tofauti kati ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu na wanamgambo wa Kikurdi wa YPG na kwamba Uturuki itaendelea kupambana na magaidi wote hao.

Uturuki inaliona kundi la YPG kama kundi la kigaidi

Jawabu hili la Uturuki limekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuonya hapo Jumapili kwamba atailemaza Uturuki kiuchumi iwapo itafanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo hao. Akimjibu mtandaoni moja kwa moja, Kalin ameandika na hapa nanukuu "Bwana Donald Trump, magaidi hawawezi kuwa washiriki na marafiki zako. Uturuki inatarajia Marekani iuheshimu ushirikiano wetu na haitaki ufunikwe na propaganda za kigaidi," mwisho wa kunukuu.

Kurdische Kämpfer schießen auf eine Drohne des IS Raqqa Rakka
Wanamgambo wa YPG wakifanya mashambulizi SyriaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Uturuki inalichukulia kundi la YPG kama magaidi waliotokana na chama cha Wakurdi cha PKK ambacho kimekuwa kikifanya mashambulizi dhidi ya Uturuki tangu 1984. Chama cha PKK kimeorodheshwa na Uturuki, Marekani na Umoja wa Ulaya kama kundi la kigaidi. Lakini katika siku za hivi majuzi Marekani imekuwa ikishirikiana na YPG kwa kuwapa usaidizi wa kijeshi na mafunzo katika kupambana na kundi la Dola la Kiislamu.

Hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo yuko nchini Saudi Arabia kwa mazungumzo kuhusu mizozo kadhaa ya Mashariki ya Kati, huku ajenda zitakazokuwa juu ikiwa mizozo ya Syria na Yemen, kitisho kutoka Iran na jibu la Saudia kuhusiana na mauaji ya mwandishi habari wa gazeti la Washington Post Jamal Khashoggi yaliyofanyika mwaka jana. 

Pompeo alizungumza na emish Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani

Rais Trump amepuuza ghadhabu za kimataifa na amesimama na mwanamfalme Mohammed Bin Salman katika mauaji ya mwandishi huyo ambaye mwili wake ulikatakatwa katika ubalozi wa Saudia nchini Uturuki.

Saudi Arabien Riad Ankunft Mike Pompeo
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike PompeoPicha: Reuters/A. Caballero-Reynolds

Kabla kuelekea Saudi Arabia Pompeo alikuwa Qatar ambapo alifanya mazungumzo na emir Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani ambapo ameitaka nchi hiyon na mataifa mengine ya Ghuba kusuluhisha tofauti zao.

"Katika taarifa yangu nimeweka wazi kwamba, tuna nguvu iwapo tutafanya kazi kwa pamoja, iwapo mizozo ni michache na tunapokuwa na changamoto moja kwenye kanda na duniani. Mizozo kati ya nchi zilizo na lengo moja inasaidia sana,"  alisema Pompeo.

Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri wote walikatisha mahusiano na Qatar Juni 2017 baada ya kuituhumu kuunga mkono ugaidi na kuwa na mahusiano ya karibu na hasimu wa Saudi Arabia, Iran.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/APE

Mhariri: Gakuba Daniel