Uturuki mwaka mmoja tangu jaribio la mapinduzi
15 Julai 2017Maafisa wameitangaza siku ya Julai 15 kuwa siku ya sikukuu ya kitaifa ya "demokrasia na umoja", kwa kuonesha kwamba kuzuiwa kwa mapinduzi ni ushindi wa kihistoria kwa demokrasia nchini Uturuki.
Watu 249 , bila la kujumuisha waliopanga njama hizo , waliuwawa wakati kikundi ambacho hakikubaliani na hali ya mambo katika jeshi kilituma vifaru mitaani pamoja na ndege za kijeshi hewani katika jaribio la matumizi ya nguvu kumuondoa madarakani Erdogan baada ya muongo mmoja na nusu madarakani.
Lakini jaribio hilo lilizuiwa katika muda wa masaa machache wakati maafisa walipojipanga na watu kumiminika mitaani kumuunga mkono Erdogan, ambaye aliwalaumu wafuasi wa mshirika wake ambae aligeuka kuwa hasimu, imamu anayeishi uhamishoni nchini Marekani Fethullah Gulen , ambaye anakana kuhusika.
Bila ya kusita , maafisa walianza kuwakamata watu wanaoshukiwa kuhusika na jaribio hilo katika operesheni kubwa kabisa kuwahi kutokea nchini Uturuki, na kuwakamata watu 50,000 na kuwafukuza kazi zaidi ya watu wengine 100,000. Erdogan pia alijiimarisha katika nafasi yake kwa kushinda kura ya maoni hapo Aprili 16 , akiimarisha madaraka yake.
Kiwango cha maadhimisho ya leo Jumamosi nchi nzima kinalenga katika kuiweka Julai 15 kusalia vichwani mwa Waturuki kama siku ya kihistoria ya taifa la kisasa lililoasisiwa mwaka 1923 kutoka katika mabaki ya himaya ya Ottoman.
"Kuanzia sasa na kuendelea, hali haitakuwa tena kama ilivyokuwa kabla ya Julai 15," Erdogan alisema katika hotuna siku ya Alhamis.
Mabadiliko ya kihistoria
Alilinganisha kushindwa huko kwa jaribio la mapinduzi na mapigano katika vita vikuu vya kwanza vya dunia mwaka 1915 katika eneo la Gallipoli ambapo vikosi vya Ottoman viliweza kuhimili mashambulizi ya wanajeshi wavamizi wa muungano katika kile kilichokuja kuwa moja kati ya simulizi za taifa la kisasa.
"Mataifa yana sehemu muhimu ya mabadiliko katika historia yake ambayo inaunda mustakabali wa baadaye. Julai 15 ni siku kama hizo kwa jamhuri ya Uturuki," amesema.
Mabango makubwa yaliyotengenezwa na rais yamezuka katika maeneo mbali mbali ya matangazo makubwa mjini Istanbul yakionesha michozi maridadi ambayo inaonesha matumio muhimu katika usiku huo wa mapinduzi, ikiwa ni pamoja na kusalimu amri kwa wanajeshi walioendesha jaribio hilo la mapinduzi.
"Kilele cha Julai 15," inasema kauli mbiu.
Upinzani walalamikia ukandamizaji
Upinzani nchini Uturuki umeweka tofauti za kisiasa kando katika usiku wa jaribio la mapinduzi. Lakini hali hii imeyeyuka tangu kura ya maoni ya tarehe 16 Aprili, ambapo wakosoaji wanamshutumu Erdogan kwa kutafuta kuwa na utawala wa mtu mmoja na kukandamiza mtu yeyote ambaye anaelezea kutoridhika kwake.
Katika hatua ya hivi karibuni, maafisa siku ya Ijumaa walitangaza kufutwa kazi kwa wanajeshi zaidi, polisi , na maafisa 7,563, ambapo karibu wanajeshi 350 waliokwishastaafu walivuliwa vyeo vyao.
Ikija katika mkesha wa maadhimisho , taarifa ilisema wale waliolengwa walikuwa "wanahusika na makundi ya kigaidi, ama makundi ambayo yana nia ya kuchukua hatua dhidi ya usalama wa taifa".
Mapema mwezi huu Uturuki pia iliwatia mbaroni mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini humo la Amnesty International pamoja na nusu dazeni ya watetezi wa haki za binadamu kwa madai ya kuhusika na kundi la kigaidi. Uturuki inaendelea kuwa chini ya hali ya hatari iliyowekwa Julai 20, ambayo imerefushwa mara tatu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Caro Robi