1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Upelelezi magazetini

26 Juni 2013

Uamuzi wa Umoja wa Ulaya kuanzisha upya mazungumzo na Uturuki na kufichuliwa mpango wa wafuasi wa itikadi kali kufanya hujuma za kigaidi kwa kutumia ndege bandia zilizosheheni miripuko ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/18wnx
Kitambulisho cha kuanzishwa mazungumzo kati ya Uturuki na Umoja wa ulayaPicha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya unapanga kuingiza kifungu chengine katika mazungumzo yanayotathmini maombi ya Uturuki kuwa mwanachama.Rasmi umoja wa Ulaya unasema mazungumzo yataanzishwa,lakini ukweli ni kwamba mazungumzo hayo hayatoanza kabla ya msimu wa mapukutiko.Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika:"Hakuna kwasasa,si waturuki na wala si wazungu wa Umoja wa Ulaya,anaevutiwa kwa dhati na uanachama kamili wa Ankara.Uturuki inalenga zaidi mashrik-inapanga kugeuka dola kuu la kiislam katika eneo hilo.Wazungu wanatambua mipango yao ya kuupanua umoja wa Ulaya imewapeleka mbali mno.Ni sawa kabisa kwamba kwa jumuia ya kujihami ya NATO,Uturuki ina umuhimu mkubwa wa kimkakati.Na pengine itafika siku Ankara inaweza kuwa mpatanishi kati ya eneo la Ulaya linalofuata imani ya kikristo na lile la Mashrik linalofuata imani ya kiislam.Lakini sio lazima iwe mwanachama kwasababu hiyo."

Nafasi ya Uturuki katika Umoja wa ulaya

EU Türkei Istanbul Konferenz 07.06.2013 Erdogan
Waziri mkuu wa Uturuki Erdogan akihutubia mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya mjini IstanbulPicha: Reuters

Wahariri wanajiuliza kama matukio ya hivi karibuni katika bustani ya Taksim ndio chanzo cha kucheleweshwa mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na Uturuki.Gazeti la "Donaukurier linaandika:"Ndo kusema kisa cha Taksim kimeikosesha Uturuki nafasi ya kukubaliwa uanachama na Umoja wa ulaya?Hasha.Kinyume kabisa.Wimbi la ghafla la maandamano limeijongeza nchi hiyo karibu zaidi na maadili ya nchi za magharibi.Kipi chengine kinachodhihirisha maadili hayo kama si wito wa kijasiri wa waandamanaji wa kituruki wa kuwa na uhuru zaidi wa kujiamulia wenyewe hatima yao?

Mipango ya kigaidi yafichuliwa

Razzia gegen Islamisten
Vikosi vya polisi vyaivamia nyumba moja mjini Munich na kutwaa masanduku ya nyaraka za siriPicha: Getty Images

Polisi nchini Ujerumani wamezivamia nyumba katika majimbo matatu ya Ujerumani,Baden Württenberg,Bavaria na Saxony baada ya kuugundua mpango wa wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam kutaka kufanya mashambulio ya kigaidi kwa kutumia ndege bandia zilizosheheni miripuko na ambazo zinarushwa kutokana nchi kavu.Gazeti la Heilbronner Zeitung linaandika:"Orodha ya mashambulio yaliyoweza kuzuiwa ni ndefu.Hata kama hali hiyo inatuliza nyoyo,lakini inatia wasi wasi pia tukizingatia kadhia nyengine.Kisa hiki kipya kimejiri katika wakati ambapo mjadala umepamba moto kuhusu kashfa ya data iliyofichuliwa na mtumishi wa zamani wa idara ya upelelezi ya Marekani Edward Snowden.Hata bila ya yote hayo,kichwa hakikosi kumzunguka mtu anapojiuliza maelezo yepi na kwa kiwango gani yameweza kukusanywa katika kufichuliwa mpango wa mashambulio kupitia ndege bandia?Ndo kusema visa vya kigaidi haviwezi kuzuwiliwa bila ya upelelezi wa jumla jamala mfano wa ule uliofanywa na idara za upelelezi za marafiki zetu wa Uingereza na Marekani.?

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo