Uturuki ni sehemu ya Ulaya
22 Machi 2007Lakini suala la uanachama wa Uturuki si jipya.Kwani takriban miaka 50 iliyopita,Uturuki ndio kwa mara ya kwanza kabisa ilipiga hodi kwenye mlango wa Umoja wa Kiuchumi wa Ulaya EEC.Mnamo mwaka 1959 Uturuki na Ugiriki ziliomba kuingia katika umoja huo wa kiuchumi.Baada ya kusitasita,umoja huo katika mwaka 1963 ulitia saini Mkataba wa Ankara,pamoja na Uturuki.Mkataba huo uliweka uwezekano wa kuipatia Uturuki uanachama baada ya miaka 17. Mwanzoni,hata Ugiriki ilikuwa na mkataba kama huo ikitazamiwa kuwa maombi ya nchi hizo mbili yatashughulikiwa wakati mmoja.Lakini Ugiriki ikapokewa mwaka 1981 kama mwanachama katika umoja huo wa kiuchumi na Uturuki ikabakia na Mkataba wa Ankara uliotoa nafasi ya kupeleka ombi la kujiunga katika Umoja wa Ulaya.
Juu ya hivyo Uturuki haikukata tamaa ya kuwa sehemu ya jumuiya hiyo na mnamo mwaka 1987 ilipeleka ombi la kuwa mwanachama kamili.Mwanzoni ombi hilo lilikataliwa hapo Desemba mwaka 1989. Badala yake ule Mkataba wa Ankara ukafufuliwa upya.Vile vile yakaanzishwa majadiliano ya kuwepo umoja wa ushuru wa forodha.Kufuatia majadiliano marefu,umoja huo ulipatikana mwaka 1996.Tangu wakati huo,Uturuki haina ruhusu ya kutoza ushuru mazao ya Umoja wa Ulaya na hushauriana na umoja huo kuhusika na ushuru wa nje.Ingawa kwa kufanya hivyo sheria za kiuchumi za Ulaya hutumika nchini Uturuki,nchi hiyo haina usemi katika Umoja wa Ulaya kuhusika na masuala ya uchumi na biashara. Kwa mujibu wa mbunge wa chama cha SPD cha Ujerumani,Lale Akgün,baadhi kubwa ya Waturuki wanahisi kuwa huo ni ubaguzi.Akaendelea kueleza kwamba Uturuki ilikubali kuwa na umoja wa ushuru wa forodha ili kurahisisha njia ya kuingia katika Umoja wa Ulaya.Uturuki haikunufaika tu kwa umoja huo wa ushuru wa forodha,bali imekubali kwa sababu imesema hatua yo yote nyingine haitoelekea kwenye Umoja wa Ulaya.
Hatimae mwaka 1997,mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg,ulipitisha uamuzi uliongojewa kwa muda mrefu juu ya uwezekano wa Uturuki kuwa mwanachama.Lakini Uturuki rasmi, haikupewa hadhi ya kuweza kuwa mwanachama. Mkutano huo ulipoamua pia kuanzisha majadiliano ya uanachama wa nchi za Ulaya ya Mashariki,basi serikali ya Uturuki ilihamakishwa.Aliekuwa waziri mkuu wa Uturuki wakati huo,Mesut Yilmaz akavunja majadiliano yaliyokuwa yakifanywa pamoja na Umoja wa Ulaya.
Majadiliano hayo yalianzishwa tena mwaka 1999. Katika mkutano wa kilele uliofanywa mjini Helsinki Desemba mwaka huo,ombi la Uturuki la kuwa mwanachama lilipokewa rasmi lakini bila ya kupewa tarehe maalum ya kuingia katika Umoja wa Ulaya.
Sababu ya kupitisha uamuzi huo ni yale mageuzi yaliyofanywa nchini Uturuki kuhusika na haki za raia.Kisheria haki za wanawake zimeboreshwa na pia uhuru na haki za binadamu zimeimarishwa. Lakini bado haijulikani ni lini au ikiwa Uturuki itapokewa kama mwanachama katika Umoja wa Ulaya. Hata hivyo mbunge Lale Akgün anaamini kuwa Uturuki ni sehemu ya Ulaya na Ulaya inaihitaji Uturuki