Uturuki kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe
10 Septemba 2015Chama hicho kimeelezea wasi wasi wake kuhusiana na ghasia zinazoongezeka kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa chama cha wafanyakazi wa Kikurdi PKK.
Chama cha Peoples Democratic HPD kimeongeza kuwa ofisi zake zimeshambuliwa mara kadhaa na kundi la wazalendo katika siku za hivi karibuni, ambapo makao yake makuu mjini Ankara yameathirika kutokana na uharibifu mkubwa kwa kuchomwa moto.
"Zaidi ya majengo 128 ya chama hicho nchi nzima yameshambuliwa," taarifa ya chama hicho imeeleza. "Zaidi ya hayo , polisi na majeshi mengine ya kulinda usalama hayakufanya chochote kuzuwia mashambulizi hayo."
Chama cha HDP wiki hii pia kimeonya kuhusu mashambulizi kadhaa yenye misingi ya kikabila yanayowalenga raia wa Kikurdi. Maduka ya wakurdi yameharibiwa na makundi ya watu, kwa mujibu wa video zilizowekwa katika mtandao wa kijamii.
Ukandamizaji wa raia
Chama hicho , ambacho kilipata asilimia 13 ya kura katika uchaguzi wa mwezi Juni mwaka huu na kuingia katika bunge kwa mara ya kwanza , pia kimeeleza wasi wasi wake kuhusiana na kile ilichosema kuwa ni "hatua za ukandamizaji" zinazotekelezwa katika eneo linaloishi Wakurdi kwa wingi la kusini mashariki, ikiwa ni pamoja na kuwekewa marufuku ya kutembea.
Katika mji wa Cizre, karibu na mpaka na Syria , amri ya kutotembea imewekwa kwa muda wa wiki.
Chama cha HDP kwa sasa kinaujumbe wake , ikiwa ni pamoja na mkuu wa chama hicho Selahattin Semirtas, ukijaribu kuingia mjini Cizre katika maandamano ya amani, lakini chama hicho kimesema wanakataliwa ruhusa ya kuingia katika mji huo na jeshi.
Mji huo na maeneo mengine katika jimbo hilo imeshuhudia mapigano makubwa kati ya wapiganaji wa PKK na majeshi ya serikali.
Kiasi ya watu 180 , ikiwa ni pamoja na raia , wanamgambo na wanajeshi wa serikali , wameuwawa ndani ya nchi hiyo tangu kuvunjika kwa makubaliano ya miaka miwili ya kusitisha mapigano Julai mwaka huu baada ya mazungumzo ya amani kukwama, kwa mujibu wa hesabu iliyotolewa na shirika la habari la Ujerumani dpa.
Ujumbe wa wabunge wazuiwa
Wizara ya mambo ya ndani ya Uturuki imesema leo, kwamba serikali hiataruhusu ujumbe wa wabunge wanawaunga mkono Wakurdi kuingia katika mji wa Cizre kusini mashariki ya Uturuki, licha ya hofu za kutokea mzozo wa kiutu unaosababishwa na amri ya wiki nzima sasa ya kutotembea ovyo iliyowekwa na jeshi.
Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Selami Altinok amewaambia waandishi habari mjini Ankara kwamba serikali haitaruhusu ujumbe wa wabunge wa chama cha Peoples Democratic HDP kuingia Cizre, na kwamba ni wajibu wa serikali kuwalinda.
Uturuki inaelekea katika uchaguzi wa mapema mwezi Novemba baada ya vyama vitano katika bunge kushindwa kukubaliana kuhusu serikali ya mseto , na kuzusha wasi wasi juu ya hali ya kutokuwa thabiti kiusalama.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / afpe
Mhariri : Yusuf , Saumu