Uturuki yaishitaki Marekani WTO
21 Agosti 2018August 10 mwaka huu rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa ataongeza mara mbili viwango vya kodi kwa asilimia 50 kwa bidhaa za chuma cha pua kutoka Uturuki na bati kwa asilimia 20 kufuatia mvutano unaoendelea kati ya nchi hizo mbili unaomhusu mchungaji wa Marekani Andrew Brunson anayeshitakiwa Uturuki kwa makosa kadhaa ukiwemo ugaidi.
Katika barua yake kwa WTO Uturuki inadai Marekani ilivunja sheria za biashara wakati ilipotangaza mwezi Juni kutoza kodi kwa asilimia 25 bidhaa za chuma cha pua na bati asilimia 10 kwa nchi nyingi isipokuwa Argentina na Australia pekee.
Kwa mujibu wa Uturuki hatua ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya Uturuki inazidiasha ukiukaji huo wa sheria za WTO.
Wiki iliyopita Uturuki ilitangaza kujibu hatua hiyo ya Marekani kwa kupandisha kodi kwa bidhaa 22 tofauti za Marekani ikiwa ni pamoja na magari, mchele , vipodozi na tumbaku.
Chini ya sheria za WTO Uturuki na Marekani sasa zinasiku 60 kumaliza mvutano huo kwa njia ya mazungumzo na kama zitashindwa kufikia muafaka basi shirika hilo litalazimika kutoa uamuzi.
Mchungaji Brunson chanzo cha mvutano
Mvutano kati ya Uturuki na Marekani umeongezeka kufuatia kuendelea kushikiliwa gerezani mchungaji wa Marekani Andrew Brunson nchini Uturuki huku pia nchi zote zikitangaziana vikwazo kwa mawaziri wa pande zote mbili. Hata hivyo Brunson amekuwa akikanusha tuhuma dhidi yake.
Vikwazo vya Marekani dhidi ya Uturuki vimesababasha kuporomoka kwa sarafu ya Lira ya nchi hiyo hali ambayo pia inaleta wasiwasi kwa mabenki ya ulaya kutokana na baadhi ya mabenki hayo kuwa na hisa katika taasisi za kifedha nchini Uturuki.
Mchungaji Brunson anayetokea North Carolina ambaye ni chimbuko la mzozo wa sasa kati ya nchi hizo washirika wa NATO uliosababisha pia kuathirika kwa masoko ya kifedha nchini Uturuki ameishi Uturuki kwa miongo miwili hadi sasa.
Ijumaa iliyopita rais Donald Trump wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari alisema kwa maoni yake anaona kuwa Uturuki wamefanya vibaya kuendelea kumshikilia Brunson kwani walipaswa kumuachia muda mrefu uliopita.
Ameongeza kuwa hawako tayari kukaa kimya wakati Uturuki inaendelea kumshikilia raia wake.
Ijumaa iliyopita mahakama ya Uturuki ililikikataa ombi la kutaka kumuachia mchungaji Brunson anayezuiliwa katika kifungo cha nyumbani .
Mwandishi: Isaac Gamba/RTRE/DPAE
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman