Uturuki yasema haiwezi kupigana peke yake nchini Syria
9 Oktoba 2014Hayo yanajiri wakati wanamgambo wa Dola la Kiislamu wakiripotiwa kutwaa thuluji moja ya mji wa Syria, Kobane, karibu na mpaka wa Uturuki. Wiki moja iliyopita, bunge la Uturuki liliipa serikali idhini ya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria. Lakini tangu wakati huo, jeshi la Uturuki halijafanya hatua yoyote kuhusu hilo.
Wanamgambo hao wa jihadi wanapigania udhibiti wa mji wa Kobane, kilomita chache tu kutoka mpaka wa Uturuki. kikosi imara cha Uturuki kilichotumwa katika mpaka huo kimekuwa kikitazama tu wakati wanajihadi hao wakipambana kuingia katikati ya mji huo.
Waziri wa Mambo ya Kigeni Mevlut Cavusoglu amesema Uturuki haiwezi kutarajiwa kuchukua hatua kivyake na akaongeza kuwa ulimwengu unahitaji kuangazia suala la kumwondoa madarakani Rais wa Syria Bashar al-Assad kando na kupigana na wanamgambo hao wenye msimamo mkali.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg anayefanya ziara mjini Ankara, Cavusoglu amesema kuwa mashambulizi yanayoendelea ya kutokea angani yanayoongozwa na Marekani dhidi ya IS hayatoshi kuleta amani nchini Syria. Anasema operesheni ya ardhini kwa ushirikiano na waasi wa Syria wanaopinga IS inastahili kuzingatiwa.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anasema eneo salama kwa ajili ya wakimbizi, pamoja na amri ya eneo la kutoruka ndege vinastahili kuwekwa nchini Syria ili Uturuki itathmini uwezekano wa kulipeleka jeshi lake nchini humo. Lakini Stoltenberg amesema suali la kuweka eneo salama la kijeshi nchini Syria halizingaitiwi na wanachama wa NATO kwa wakati huu.
Wakati huo huo, jenerali mstaafu wa Marekani John Allen, ambaye ni mjumbe maalum wa Marekani katika jeshi la muungano dhidi ya IS, anatarajiwa kuwasili Ankara ili kuishawishi Uturuki kuchukua msimamo imara. Wapiganaji wa Kikurdi wameonakana kuendelea kudhibiti sehemu kubwa ya mji wa Kobane, wakati Marekani ikiendeleza mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya IS. Jeshi la Marekani limesema ndege zake za kivita pamoja na ndege zisizoruka na rubani zilifanya mashambulizi matano kusini mwa Kobane, na kuharibu kabisa kambi ya mafunzo ya IS, jengo moja na magari mawili.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo