1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanahabari maarufu ni miongoni mwa wanaotakiwa kukamatwa

Admin.WagnerD25 Julai 2016

Serikali ya Uturuki imetoa waranti ya kukamatwa waandishi wa habari 42 ikiwa ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusiana na jaribio la mapinduzi lililoshindwa.

https://p.dw.com/p/1JVOr
Rais wa Uturuki,Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki,Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/U.Bektas

Miongoni mwa wale wanaotakiwa kukamatwa ni pamoja na mwandishi wa habari maarufu nchini humo Nazli Ilicak ambaye alifutwa kazi katika gazeti linaloegemea serikali la Sabah Daily mnamo mwaka 2013 kutokana na kuwakosoa mawaziri waliokuwa wakihusishwa na kashfa ya rushwa.

Hata hivyo hadi sasa hakujawa na dalili zinazoashiria kutiwa mbaroni kwa mwandishi yeyote kufuatia kutolewa waranti huo wa kukamatwa kwao.

Serikali ya Uturuki imekuwa ikimshutumu kiongozi wa kidini aliyeko uhamishoni nchini Marekani Fethullah Gulen kwa kuwa nyuma ya kashfa hiyo ya rushwa na pia njama ya mapinduzi.

Gazeti la Hurriyet limesema waranti huo ambao ni wa kwanza kuwalenga waandishi wa habari kuhusiana na msako unaoendelea dhidi ya wale wote wanaodaiwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi la Julai 15, ulitolewa na afisa mwendesha mashitaka wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini humo Irfan Fidan. Mwendesha mashitaka huyo amesema operesheni ya kuwatia mbaroni waandishi hao wa habari tayari ilikuwa imeanza ingawa mwanahabari huyo Ilicak hakukutwa nyumbani kwake mjini Istanbul na yawezekana akawa katika mapumziko binafisi katika ufukwe wa bahari ya Aegean.

Utawala wa Rais Erdogan umekuwa ukikosolewa hata kabla ya jaribio hilo la mapinduzi kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, shutuma ambazo serikali hiyo imezikanusha. Na waziri wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu amesema katika mahojiano na kituo binafsi cha Televisheni kuwa baadhi ya mabalozi wataondolewa katika vituo vyao vya kazi kuhusiana na jaribio hilo la mapinduzi.

Maandamano yafanyika kulaani jaribio la mapinduzi

Wakati huohuo maelfu ya wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki wakiungana na baadhi ya

Baadhi ya waandamanaji mjini Istanbul
Baadhi ya waandamanaji mjini IstanbulPicha: DW/K. Akyol

wafuasi wa chama tawala waliaandamana hapo jana mjini Istanbul huku wakipeperusha bendera kulaani jaribio hilo la mapinduzi katika taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO ambalo limepitia mapindizi kadhaa ya kijeshi katika miongo iliyopita.

Maandamano hayo yaliandaliwa na chama cha upinzani cha Republican Peoples Party ambacho kiko karibu zaidi na majenerali wa jeshi ambao hawajifungamanishi na misimamo ya kidini ambao wamekuwa na sauti ndani ya jeshi.

" Jaribio hilo la mapinduzi lilifanywa kinyume cha misingi ya utawala wa kisheria inayoongoza nchi yetu" alisikika akisema kiongozi wa chama cha Republican Peoples Party, Kemal Kilicdaroglu.

Hata hivyo kiongozi huyo hakumkosoa moja kwa moja Rais Erdogan ingawa alisisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uhuru wa kukusanyika na hatari ya kuwepo kwa utawala wa kidikiteta na kimabavu.

Licha ya mgawanyiko mkubwa wa kisiasa uliopo nchini Uturuki, Meya wa mji wa Istanbul na viongozi wengine wa chama tawala cha Justice and Development Party waliungana na waandamanaji kutoka upinzani kulaani jeshi kuingilia masuala ya kisiasa.

Uturuki hivi sasa iko katika hali ya wasiwasi wa kiusalama na tayari serikali ya nchi hiyo imetangaza hali ya hatari italayodumu kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo pia imewatia mbaroni zaidi ya watu 13,000, miongoni mwao wanajeshi 9,000, majaji na waendesha mashitaka 2,100 pamoja na maafisa wa polisi 1,485 tayari wametiwa mbaroni nchini Uturuki wakihusishwa na mipango ya jaribio hilo la mapinduzi.

Uturuki pia imekuwa ikiandamwa na mashambulizi kadhaa ya mabomu na mashambulizi mengine yanayodaiwa kufanywa na kundi la itikadi kali la Dola la Kiislamu.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE/ APE

Mhariri: Iddi Ssessanga