1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatuhumu 'hatua za ubabe'' za Ufaransa

Saleh Mwanamilongo
14 Agosti 2020

Uturuki inaishutumu Ufaransa kuhusu hatua yake ya kutuma meli za kivita kwenye eneo linalozozaniwa baina yake na Ugiriki kwenye bahari ya Mediterania.

https://p.dw.com/p/3gz4k
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu na mwenzie wa Uswissi Ignazio Cassis,ijumaa mjini Geneva,Uswisi.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu na mwenzie wa Uswissi Ignazio Cassis,ijumaa mjini Geneva,Uswisi.Picha: picture-alliance/Keystone/P. Schneider

 Uturuki inaishutumu Ufaransa kuhusu hatua yake ya kutuma meli za kivita kwenye eneo linalozozaniwa baina yake na Ugiriki kwenye bahari ya Mediterania mashariki. Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamekutana Ijumaa kwa njia ya video ili kuujadili pia mzozo huo baina ya Ugiriki na Uturuki. 

Kwenye mkutano wa pamoja na mwenzake wa Uswisi mjini Geneva hii leo, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesema kwamba Ufaransa ni lazima isitishe hatua zitakazochangia kukuza mzozo huo wa Mediterania mashariki.

''Ikiwa tunataka suluhisho la mzozo huu,Uswisi imechukuwa msimamo wa kati na usiopendelea upande wowote kwa ajili ya upatanishi. Kimsingi tumekubali pendekezo la upatanishi. Tunategemea kulifanyia kazi pendekezo hilo, lakini Ufaransa inatakiwa kujizuwiya na hatua zitakazochochea mzomzo.'',alisema Cavusoglu.

Cavusoglu aliendelea kusema Ufaransa haitofanikiwa ikiwa itachukuwa hatua za ubabe. Meli ya utafiti ya Uturuki ilianza shughuli ya utafutaji mafuta na gesi asilia Jumatatu, hatua iliyoikasirisha Ugiriki. Pia kuna wasiwasi kuhusu Cyprus juu ya haki za utafutaji mafuta za mahasimu wao.

Mkutano wa EU kwa ajili ya mzozo wa mediterania

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitaka Uturuki kusitisha shughuli ya utafutaji wa mafuta na gesi katika eneo la maji linalozozaniwa karibu na visiwa vya Cyprus. Na kuelezea kwamba Ufaransa inatuma jeshi lake Mediterania.

Türkisches Forschungsschiff Oruc Reis zur Gaserkundung im Mittelmeer
Picha: picture-alliance/AP/DHA/I. Laleli

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema suluhu pekee kwa mzozo wa Mediterania mashariki ni mazungumzo. Erdogan amesema kwamba malengo ya Uturuki ni kuhakikisha kuwa haki ya kila taifa katika ukanda wa Mediterania Mashariki inaheshimiwa.

Rais Erdogan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wamekutana leo kwa njia ya video ili kujadili mzozo huo wa Mediterania mashariki baina ya Uturuki na Ugiriki. Duru zinaelezea kwamba nchi za Umoja wa Ulaya zimeunga mkono msimamo wa Ugiriki.