Vatican: Papa Francis hatohudhuria mkutano wa COP28
29 Novemba 2023Matangazo
Hayo yameelezwa na msemaji wa makao makuu ya kanisa katoliki mjini Vatican, Matteo Bruni, alipozungumza na waandishi habari jana jioni.
Afisa huyo amesema licha ya kuimarika kwa hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa kiroho, Baba Mtakatifu Francis hatoweza kufanya ziara yake ya siku tatu huko Umoja wa Falme za Kiarabu kutokana na ushauri wa madaktari.
Papa Francis alipata maambukizi ya mafua na uvimbe kwenye mapafu mwishoni mwa juma.
Wiki hii alikuwa amepangiwa kuhudhuria mkutano wa COP28 na kuwa kiongozi wa kwanza wa kanisa katoliki kutoa hotuba mbele ya kongamano hilo la mazingira linalotafuta njia za kulishughulikia janga la mabadiliko ya hali ya hewa.