1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya watu maarufu vilivyotokea 2021

28 Desemba 2021

Kuanzia kifo cha mwanamfalme wa Uingereza Philip hadi kifo cha mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 1984 Desmond Tutu.

https://p.dw.com/p/44uqU
Desmond Tutu und Queen Elizabeth II
Picha: SEAN DEMPSEY/AFP

Hivi ni baadhi tu ya vifo vya watu mashuhuri au maarufu vilivyotokea mwaka 2021.

Januari 16, Phil Spector aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Phil  alileta mageuzi makubwa katika muziki aina ya Pop, lakini pia alifungwa jela mnamo 2009 kwa hatia ya mauaji.

Wiki moja baada ya kifo chake, mtangazaji maarufu wa Marekani Larry King aliyewahoji watu wa tabaka mbalimbali pia alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 87.

Februari 5, muigizaji mkongwe wa Canada Christopher Plummer aliyetamba kwenye filamu ya "The Sound of Music” aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 91.     

George Schultz, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani chini ya utawala wa Ronald Reagan, na ambaye alisaidia kumaliza Vita Baridi akafa siku iliyofuata yaani Februari 6 akiwa na umri wa miaka 100.

Rais wa zamani wa Argentina Carlos Menem naye akafa Februari 14 akiwa amefikisha umri wa miaka 90.

Mumewe Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza ambaye pia ni mwanamfalme Philip aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 99.
Mumewe Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza ambaye pia ni mwanamfalme Philip aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 99.Picha: Anwar Hussein/PA Images/imago images

Lawrence Ferlinghetti, mmoja wa watunzi mahiri wa mashairi wa kizazi cha The Beat, akaenda jongomeo siku nane baadaye akiwa na umri wa miaka 101.

Michael Somare ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Papua New Guinea na aliyetajwa kuwa baba wa taifa hilo vilevile alifarakana na dunia mnamo Februari 26 akiwa amebugia chumvi ulimwenguni kwa miaka 84.

Kwa wapenzi wa muziki miondoko ya Reggae, Machi 2, ni siku iliyowaacha wakiwa na kihoro. Gwiji wa reggae Bunny Wailer aliipungua dunia mkono wa buriani siku hiyo akiwa na umri wa miaka 73.

Machi 12, mfalme wa jamii ya Zulu Afrika Kusini kwa jina Goodwil Zwelithini naye akatangulia mbele ya haki akiwa na umri wa miaka 72.

Nchini Madagascar, wingu la simanzi lilitanda mnamo Machi 28, wakati kiongozi wa zamani wa kisiwa hicho cha Bahari Hindi Didier Ratsiraka ambaye pia alianzisha mapinduzi ya kisosholisti alipoaga dunia akiwa na umri wa miaka 84.

Rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda ni miongoni mwa watu mashuhuri walioaga dunia mwaka 2021.
Rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda ni miongoni mwa watu mashuhuri walioaga dunia mwaka 2021.Picha: Alexander Joe/AFP/Getty Images

 Aprili 9, kifo kikabisha hodi katika hedikota ya malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza na kumchukua mume wake Mwanamfalme Philip akiwa na umri wa miaka 99.  

Aprili 20, rais wa Chad Idriss Deby naye akaaga dunia akiwa na umri wa miaka 68 siku chache tu baada ya kuchaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa sita     

Nchini Zambia, rais wa zamani Kenneth Kaunda aliyetajwa kuwa Gandhi wa Afrika naye alituacha mnamo Juni 17 akiwa na umri wa miaka 97.     

Agosti 24, rais wa zamani wa Chad Hissene Habre alifariki kutokana na COVID-19 akiwa na umri wa miaka 79. Alifariki wakati akitumikia kifungo cha Maisha jela nchini Senegal kufuatia hatia dhidi ya ubinadamu.

Rais wa muda mrefu wa Algeria Abdelaziz Bouteflika, aliaga dunia Septemba 17.

Beerdigung I  Abdelaziz Bouteflika
Jeneza lililoubeba mwili wa rais wa muda mrefu wa Algeria Abdelaziz Bouteflika likisafirishwa kwa mazishi.Picha: Mousaab Rouibi/AA/picture alliance

Nchini Kenya, aliyeshikilia rekodi ya dunia katika moja kati ya riadha Agnes Tirop alikufa Oktoba 13 baada ya kudungwa kisu. Baadaye mumewe alishtakiwa kwa madai ya kuhusika na mauaji hayo.   

Colin Powell aliyekuwa waziri wa kwanza mweusi wa Marekani kuongoza wizara ya mambo ya nje pia aliaga dunia mwaka huu.

Nchini Afrika Kusini, Novemba 11, rais wa zamani na wa mwisho katika enzi za ubaguzi wa rangi nchini humo de Klerk aliaga dunia.

Na hatimaye kifo cha hivi karibuni Zaidi miongoni mwa watu mashuhuri walioaga dunia mwaka 2021 ni chake Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini aliyeaga dunia Disemba 26 akiwa na umri wa miaka 90. Tutu anafahamika kama mpiganiaji dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukikwaji wa haki

(AFPE)