Vijana wa Afrika wataka hatua zaidi kulinda mazingira
29 Novemba 2023Afrika inachangia asilimia 4 tu katikka uzalishaji wa kaboni duniani, ikilinganishwa na mataifa ya Ulaya na Amerika Kaskazini, pamoja na China. Hata hivyo, bara hilo bila shaka ndilo lililoathiriwa zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inaendelea kukabiliwa na mfululizo wa ukame, mafuriko, vimbunga na majanga mengine yanayohusiana na hali ya hewa.
Vijana wa Afrika wamesema hawana cha kutarajia na sasa wanadai hatua madhubuti: Mapema mwezi Oktoba, karibu vijana 150 kutoka barani kote walikutana katika mji mkuu wa Kamerun, Yaounde, katika Kongamano la Kwanza la Vijana kuhusu Ufadhili wa Mabadiliko Afrika (YOFAFA).
Wengi wanatumai mkutano huu utazingatiwa kama wakati wa kihistoria kwa ushiriki wa vijana juu ya hatua za kimazingira, ambapo vijana wa Afrika walitoa wito kwa nchi zilizoendelea kutoa fedha zaidi kusaidia bara hilo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Afrika: Bara la joto kali
Kupunguza athari za ongezeko la joto duniani ni mpambano mgumu sana wa kupanda mlima katika sehemu kubwa ya Afrika: Halijoto katika majimbo tete katika bara zima tayari iko juu kwa sababu ya maeneo yao ya kijiografia.
Hata hivyo, ripoti ya Hali ya Hewa barani Afrika 2022 inaonyesha kwamba kasi ya ongezeko la joto barani Afrika imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miongo ya hivi karibuni, huku hali ya hewa na hatari zinazohusiana na hali ya hewa zikizidi kuwa mbaya kila mwaka.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wasema ulimwengu "unakwenda mrama" upunguzaji gesi ukaa
Kufikia 2040, mataifa dhaifu yanaweza kukabiliwa na siku 61 za joto kali kwa mwaka, la zaidi ya nyuzi 35 kwa wastani - mara nne zaidi ya nchi nyingine kote ulimwenguni.
Serikali nyingi za Kiafrika, wakati huo huo, zinalazimika kutegemea misaada ili kutoa hata huduma za msingi kwa raia wao. Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ingeonekana, jambo la kando kabisaa katika muktadha huu.
Ukosefu wa muda mrefu wa fedha za tabianchi
Hii ndiyo sababu ufadhili wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika umekuwa kipaumbele kikuu kwa vijana wa Afrika, kwa kuzingatia kuonyesha miradi ambayo itasaidia watu kuishi katika wakati ujao wa joto kali sana.
Lakini ukosefu wa muda mrefu wa ufadhili wa kukabiliana na hali hiyo unafanya kuwa vigumu kustahimili barani humo.
Wakati wa mkutano wa siku mbili wa YOFAFA nchini Cameroon, vijana wa Kiafrika walitetea kuongezwa kwa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wakitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "kujitolea zaidi ya mara mbili ya fedha za kukabiliana na hali barani Afrika," kulingana na waandaaji wa mkutano huo.
Suluhu za ndani zahitaji ufadhili wa kimataifa
Wakati huo huo, tayari kuna mawazo mengi ya kuongoza makabiliano ya tabianchi barani Afrika.
Nchini Kamerun, Mbong Kimbi kutoka Muungano wa Afrika wa Upatikanaji wa Nishati Endelevu amekuwa akifanya kazi na jamii za wakulimwa kuwasaidia kuzowea uhalisia wa mvua zisizotabirika na udongo unaoharibika.
Soma pia: Mzozo wa Israel na Hamas utaathiri vipi mkutano wa COP28?
“Tunawafundisha wakulima jinsi ya kuzalisha mbolea ya kibaiolojia na dawa ya kunyunyizia mimea, jinsi ya kuzitumia kwa usahihi katika mashamba yao, na kufuatilia, kwa sababu mbolea za mimea zina kemikali nyingi ambazo zitasaidia udongo na hivyo kusaidia mazao yao,” Kimbi alifafanua. "Matokeo ya mwaka jana yalikuwa mazuri sana kwa awamu ya majaribio ya programu. Tunakwenda katika awamu inayofuata, lakini moja ya matatizo tuliyo nayo ni kupata ufadhili."
Hakika, upungufu wa kulipia miradi muhimu ni mkubwa - na unaongezeka.
Kulingana na Augustine Njamnshi, mkurugenzi mtendaji wa Muungano wa Afrika wa Upatikanaji wa Nishati Endelevu, Afrika inahitaji zaidi ya dola bilioni 50 kila mwaka hadi 2030 ili kukabiliana vya kutosha na changamoto zake za hali ya hewa.
Hata hivyo kati ya 2019 na 2020, bara hilo lilipokea kiasi cha dola bilioni 11.4 tu kwa ajili hiyo, na hivyo kuacha upungufu mkubwa.
"Kufuatia ripoti ya Pengo la Marekebisho ambayo ilichapishwa siku chache zilizopita, pengo la sasa la urekebishaji wa fedha sasa linakadiriwa kuwa dola bilioni 194 hadi bilioni 366 kwa mwaka," Njamnshi alisema.
Ukame mkubwa na mafuriko
Madhara ya upungufu huo mkubwa yanaweza kuonekana kote barani Afrika. Kama Shirika la Fedha la Kimataifa lilivyoripoti, mataifa dhaifu katika Ulimwengu unaoendelea yanakabiliwa zaidi na mishtuko inayohusiana na hali ya hewa kuliko nchi nyingine: Kila mwaka, mara tatu zaidi ya watu wanaathiriwa na majanga ya asili katika mataifa hayo hatari, na zaidi ya mara mbili ya sehemu ya wakazi wao kuhamishwa na matukio kama haya.
Mwanaharakati wa mazingira wa Kenya, Anna Shampi anazungumza kwa uwazi juu ya kile ambacho mabadiliko ya tabianchi yameifanyia jamii yake na kutoa picha mbaya kwa siku zijazo: "Tumekuwa na misimu sita ya mvua zilizofeli, na hii ina maana kwamba kila mwaka wafugaji wamekuwa wakipoteza ng'ombe wao, ambao ndio njia yao ya kujikimu."
Alisema kuna haja ya kuja na miradi ya kuwezesha jamii kukabiliana na mabadiliko hayo, lakini, hadi sasa, inaonekana kuna mikakati kidogo kwa upande wa serikali.
Kuwania rasilimali zinazopungua kunaweza pia kusababisha mapigano kati ya jamii za wakulima na wafugaji, Shampi alisema.
"Wakati wowote mvua ikinyesha - sijui kwa sababu fulani - inashuka kwa nguvu," alisema. "Siku zote ni mafuriko. Ikiwa tuna ukame, ni wa hali ya juu, ikiwa tuna mvua, pia iko upande uliokithiri, upande wa mafuriko. Nyumba zetu nyingi ni za muda, kwa hivyo zinaishia kusombwa."
Mapambano ya kulinusuru bara
Hali ya Shampi ni mojawapo ya masimulizi mengi yanayofanana kote barani Afrika. Hali mbaya ya ufadhili inazielemea sana hazina za mataifa mengine ya Kiafrika pia.
Soma pia: Umoja wa Mataifa wasema mabadiliko ya tabia nchi ni kitisho cha afya
Kuna mabadiliko fulani yanayoonekana - ingawa inaweza kuwa suala lililokuja kuchelewa sana: nchi 11 za Afrika sasa zinatumia mara tano zaidi kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi kuliko zinavyotumia katika huduma za afya, alisema Njamnshi.
Lakini wakati yakikosekana kufikia malengo, hii inaweza tu kuwa sana tone katika bahari.
Ndio maana vijana waliokusanyika Yaounde walisema COP28, inayotarajiwa kufanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia mwishoni mwa Novemba hadi katikati ya Desemba, inapaswa kushughulikia tofauti hizi na kuongeza kwa kiasi kikubwa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa bara hilo ambalo linahusika kidogo sana na mabadiliko ya tabianchi lakini lililoathiriwa zaidi na mabadiliko hayo.