1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Vikosi vya Syria vyawashambulia raia kiholela"

19 Septemba 2012

Amnesty International inasema vikosi vya serikali ya Syria vimefanya mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia kutokea angani na vimetumia mizinga, huku pia waasi wakiripotiwa kuteka kituo cha mpakani mwa Uturuki.

https://p.dw.com/p/16BQ4
Hali kufuatia mapambano makali kusini mwa Damascus.
Hali kufuatia mapambano makali kusini mwa Damascus.Picha: AP

Kwa mujibu wa mtafiti mwandamizi wa masuala ya dharura wa Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu Amnesty International ambaye Donatella Rovera alitembelea miji na vijiji 26 nchini Syria kati ya Augusti 31 na Septemba 11, kushambuliwa huko ovyo kwa raia kunakiuka vifungu vya msingi vya sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu kwa kuwa yanashindwa kupambanuwa kati ya maeneo ya kiraia na yale ya kijeshi.

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London limesema wengi wa wahanga ni watoto ambao wamekufa katika mashambulizi yanayowakuta watu wakiwa majumbani mwao au wakati wakijaribu kutafuta hifadhi kujikinga na mashambulizi na hayo.

Shirika hilo la Amnesty pia limewashutumu wapiganaji wa waasi ambapo imesema pia wamekiuka haki za binaadamu.

Kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binaadamu takrkiban watu 170 wameuwawa hapo jana nchini kote Syria wengi wao wakiwa katika viunga vya Damascus.

Waasi wateka kituo cha mpaka na Uturuki

Inaripotiwa kwamba waasi wa Syria wamekiteka kituo cha mpaka wa Syria na Uturuki na kuiteremsha chini bendera ya Syria baada ya mapigano makali hapo jana kati ya waasi na vikosi vya serikali kuwania udhibiti wa kituo hicho cha Tal Abyad.

Waasi wa Jeshi Huru la Syria wakati wa mapambano na jeshi la serikali katika mji wa Allepo.
Waasi wa Jeshi Huru la Syria wakati wa mapambano na jeshi la serikali katika mji wa Allepo.Picha: AP

Waasi wa Syria wanavidhibiti vituo vengine kadhaa vya mpaka wa kuingilia Uturuki lakini inaaminika kwamba hii ni mara ya kwanza kujaribu kuteka eneo la mpaka katika jimbo la kaskazini la Raqqa.

Wakati hayo yakijiri Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi amewasili Damascus leo hii kwa mazungumzo na Rais Bashar al Assad baada ya kupendekeza kutumwa kwa waangalizi wa kanda katika nchi hiyo iliokumbwa na vita.

Salehi amewaambia waandishi wa habari kwamba atakutana pia na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem.

Iran yataka kukomeshwa msaada kwa waasi

Ziara yake hiyo inakuja kufuatia mkutano wa Cairo uliofanyika hapo Jumatatu wa kundi la mawasiliano la kanda kwa mzozo wa Syria ambao pia ulihudhuriwa na mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu Lakhdar Brahimi.

Rais Mohamed Mursi wa Misri akikutana na Waziri wa Mambo ya Njew wa Iran Ali Akbar Salehi mjini Cairo.
Rais Mohamed Mursi wa Misri akikutana na Waziri wa Mambo ya Njew wa Iran Ali Akbar Salehi mjini Cairo.Picha: Reuters

Salehi hapo jana alitowa wito kwa pande zote husika nchini Syria kusitisha mapambano na umwagaji damu akisisitiza utatuzi wa amani kwa mzozo huo bila ya uingiliaji kati kutoka nje pamoja na kusitishwa kwa msaada wa kifedha,kijeshi na mafunzo kwa waasi wa Syria.

Serikali ya Iran inapandekeza kwamba kundi la mawasiliano la kanda kwa mzozo huo wa Syria la nchi nne za Misri,Iran,Saudi Arabia na Uturuki litume waangalizi nchini Syria katika juhudi za kukomesha umwagaji damu.Iran imekanusha vikali shutuma kwamba inatowa msaada wa kijeshi kwa utawala wa Assad.

Upinzani unasema zaidi ya watu 27,000 wameuwawa katika mzozo huo wa Syria wakati Umoja wa Mataifa unasema watu waliouwawa kutokana na mzozo huo ni 20,000.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf