Vikosi vya Ufaransa vyamuuwa mkuu wa IS ukanda wa Sahel
16 Septemba 2021Ni katika operesheni iliyofanywa na wanajeshi wa Ufaransa, na kifo cha al Sahrawi kimetangazwa leo Alhamisi 16.09.2021 na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Akithibitisha kifo cha mkuu huyo wa kundi linalojiita dola la kiislamu katika ukanda wa Jangwa la Sahara (ISGS), Rais Emmanuel Macron kupitia ujumbe wake wa Twitter amesema, kuuwawa kwa Sahrawi ni mafanikio mengine makubwa katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi kwenye ukanda wa Sahel. Hata hivyo Rais Macron hakutaja eneo wala kutoa maelezo ya kina kuhusu operesheni hiyo.
Kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Ufaransa Florence Parly naye kupitia mtandao wa Twitter, amesema , Sahrawi aliuwawa baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa Ufaransa wa operesheni Barkhane ambao wanapambana na makundi ya jihadi kwenye ukanda wa Sahel. Sahara Adnan Abu Walid al-Sahrawi ndiye aliyeendesha mauaji ya wafanyakazi wa misaada ya kiutu wa Ufaransa mnamo mwaka 2020. Alikuwa akitafutwa pia na Marekani kutokana na mashambulizi ya mwaka 2017 yaliyowalenga wanajeshi wa Marekani huko Niger.
Mwaka 2015, Sahrawi alianzisha kundi la dola la kiislamu katika Jangwa la Sahara- ISGS ambalo linalaumiwa kwa mashambulizi mengi ya jihadi katika mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso. Eneo la mpaka linalohusisha nchi hizo tatu limekuwa likilengwa na kundi hilo pamoja na kundi jingine lenye lenya mafungamano na Al-Qaeda, la GSIM
Aliwahi kuwa mwanachama wa Al-Qaeda
Awali Marekani ilitangaza zawadi ya dola milioni 5 za kimarekani kwa watakaotoa taarifa juu ya mienendo ya Sahrawi. Kiongozi huyo wa kundi la dola la Kiislamu katika Jangwa la Sahara, ambaye ni mwanachama wa zamani wa chama cha vuguvugu cha ukombozi wa Sahara Magharibi cha Polisario alijiunga na Al-qaeda na pia aliwahi kuliongoza kundi la Mujao la Mali lililohusika kuwateka nyara wafanyakazi wa kigeni wa mashirika ya kutoa misaada nchini Algeria, na kundi la wanadiplomasia wa Algeria mnamo mwaka 2012.
Jeshi la Ufaransa, limeshawauwa wanachama kadhaa wa ngazi ya juu wa ISGS, chini ya mkakati wao unaowalenga viongozi wa jihadi tangu majeshi ya nchi hiyo yalipoingilia kati Mali mwaka 2013. Mnamo mwezi Juni mwaka huu, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza kupunguza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wa operesheni Barkhane kwenye ukanda wa Sahel baada ya kuwepo katika eneo hilo kwa takribani miaka minane.