Vikosi vya Urusi vyabadili mwelekeo wake Bakhmut
25 Machi 2023Taarifa iliyotolewa Jumamosi na wizara hiyo, pamoja na mkuu wa jeshi la Ukraine, Valerii Zaluzhnyi, imeeleza kuwa mashambulizi ya Urusi huko Bakhmut yamekwama na wanajeshi wa Ukraine wamezidi kujiimarisha. Aidha, vikosi vya Urusi vinaelekezea juhudi zao kwenye mji wa Avdiivka, kusini mwa Bakhmut na Kremina-Svatove, eneo la kaskazini.
Kulingana na taarifa hiyo, Urusi inaonekana kurejea kwenye nafasi ya ulinzi zaidi baada ya juhudi zao za mashambulizi yaliyoanza Januari, kushindikana.
Jaribio la Urusi kuiteka Bakhmut lashindwa
Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema jaribio la Urusi kuuteka mji wa Bakhmut limeshindwa kutokana na msuguano uliozidishwa na mzozo wa ndani kati ya wanajeshi wa Urusi na wapiganaji wa kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner ambao wote wanahusika kusambaza wapiganaji kwenye eneo hilo.
Hata hivyo, sehemu inayoizunguka Bakhmut bado ni moja ya maeneo magumu zaidi katika uwanja wa mapambano na Uingereza imesema inatambua kuwa Ukraine pia imepata majeruhi wengi kutokana na mapigano ya Bahkmut.
Wakati huo huo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema mashambulizi yanayotarajiwa dhidi ya vikosi vya Urusi hayawezi kutokea sasa kwa sababu nchi hiyo haina silaha, vifaa wala risasi.
Zelensky ameitoa tathmini hiyo katika ripoti iliyochapishwa Jumamosi na gazeti la kila siku la Japan, Yomiuri Shimbun. "Bado hatuwezi kuanza. Bila vifaru na makombora, na hakuna askari jasiri anayeweza kupelekwa eneo la mapambano," Zelensky aliliambia gazeti hilo, katika mahojiano yaliyofanywa siku ya Alhamisi.
Spika wa bunge la Urusi ataka ICC ipigwe marufuku Urusi
Ama kwa upande mwingine, Spika wa Bunge la Urusi Vyacheslav Volodin amependekeza kupigwa marufuku shughuli za Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC nchini humo.
Volodin, mshirika wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin, ametoa matamshi hayo baada ya mahakama hiyo kutoa waranti wa kukamatwa Putin kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita, kutokana na kuwapeleka Urusi mamia ya Watoto kutoja Ukraine.
"Sheria inapaswa kutungwa itakayokataza shughuli za aina yoyote za ICC kwenye eneo la nchi yetu," alisisitiza Volodin. Spika huyo wa Bunge la Urusi pia amesema mtu yeyote atakayeisaidia au kuiunga mkono mahakama ya ICC ataadhibiwa.
Volodin amedokeza kwamba Marekani ilitunga sheria ya kuwazuia raia wake kuhukumiwa na mahakama hiyo, na kwamba Urusi inapaswa kufanya vivyo hivyo.
New Zealand yaitaka China kutoipatia Urusi silaha
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand, Nanaia Mahuta ameelezea wasiwasi wake kuhusu China kuipatia silaha Urusi katia vita vyake dhidi ya Ukraine.
Katika mkutano wake na Waziri mwenzake wa China, Qin Gang, Mahuta amerudia msimamo wa serikali yake kulaani "uvamizi haramu" wa Urusi nchini Ukraine.
Ofisi ya Habari ya Mahuta siku ya Jumamosi ilisema matamshi hayo yametolewa mjini Beijing, siku kadhaa baada ya Rais wa China, Xi Jinping kumalizia ziara yake ya siku tatu mjini Moscow.
(AFP, DPA, Reuters)