Viongozi COP26 waahidi juhudi mpya kuokoa misitu ya dunia
2 Novemba 2021Mkutano muhimu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa umesikia miito katika siku yake ya kwanza, kwa mataifa makubwa kiuchumi kutimiza ahadi zao za kutoa msaada wa kifedha kusaidia kushughulikia mzozo wa tabianchi, huku wachafuzi wakubwa India na Brazil zikitoa ahadi mpya za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.
Viongozi wa dunia, wataalamu wa mazingira na wanaharakati wote wamehimiza kuchukuliwa hatua thabiti kusitisha ongezeko la joto la dunia, ambalo linatishia mustakabali wa sayari, katika siku ya kwanza ya mkutano wa kilele wa wiki mbili, COP26, unaofanyika katika mji wa Glasgow nchini Scotland.
Soma pia: Ulimwengu waelekeza macho Glasgow COP26
Jukumu linalowakabili wajumbe wa majadiliano lilifanywa kuwa gumu hata zaidi na kushindwa kwa kundi la G-20 la mataifa makubwa zaidi ya viwanda duniani, kukubaliana juu ya ahadi mpya kubwa mwishoni mwa wiki.
Mataifa ya G-20 yanahusika na karibu asilimia 80 ya utoaji wa gesi chafu duniani, na kiwango sawa cha gesi ya kaboni inayotokana na kuchomwa kwa nishati ya kisukuku ambayo chanzo kikuu cha kuongezeka kwa joto la dunia, linalosababisha ongezeko la mawimbi ya joto, ukame, mafuriko na dhoruba.
Mkutano wa COP26 uliocheleweshwa kwa mwaka moja kwa sababu ya janga la Covid-19, unalenga kubakisha hai shabaha ya kupunguza joto la dunia kwa nyuzi 1.5 za celsius, juu ya viwango vya kabla ya mapindizi ya viwanda.
Soma pia: Barua kutoka Dar: Je mkutano wa COP26 italeta ahueni ?
Ili kufanikisha hilo, mkutano huo unahitaji kupata ahadi kubwa za kupunguza uchafuzi, kutoa mabilioni ya ufadhili wa tabianchi kwa mataifa yanayoendelea, na kukamilisha sheria za utekelezaji wa azimio la Paris la mwaka 2015, lililosainiwa na karivu mataifa 200.
"Endapo ahadi hazitatimia kufikia mwishoni mwa COP hii, mataifa laazima yapitie upya mipango na sera zao za kitaifa kuhusu mazingira, siyo kila miaka mitano, bali kila mwaka, kila wakati, hadi uhifadhi wa nyuzi joto 1.5 utakapohakikishwa," alisema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Ahadi zisizotimia
Zaidi ya viongozi 100 wa dunia waliahidi jana jioni kusitisha na kupindua uharibuji wa misitu na ardhi kufikia mwishoni mwa muongo huu, huku zaidi ya dola bilioni 19 zikiahidiwa kuimarisha mpango huo, ambao unaungwa mkono na mataifa yakiwemo Brazil, China, Congo, Urusi na Marekani.
Mwenyekiti wa mkutano huo wa kilele, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson, alisema makubaliano kuhusu uharibifu wa misitu yalikuwa muhimu kwa lengo kuu la kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi 1.5 za celsius.
Soma pia: COP26: Viongozi wa dunia kujadiliana kukabili ongezeko la joto
Mnamo mwaka 2009, mataifa yalioendelea na yanayohusika zaidi na ongezeko la joto duniani yaliahidi kutoa msaada ya dola bilioni 100 kila mwaka kufikia 2020, kuyasadia mataifa maskini kushughulikia madhara.
Lakini ahadi hiyo haikutimizwa, na kusababisha hali kutoaminiana na usitaji wa baadhi ya mataifa kuharakisha upunguzaji wa gesi chafuzi.
Chanzo: Mashirika.