1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi walaani vurugu zilizoibuka mjini Amsterdam

8 Novemba 2024

Viongozi wa Ulaya wameungana na Israel na Uholanzi kulaani vurugu zilizoibuka baada ya mechi kati ya timu za Maccabi Tel Aviv na Ajax ya Amsterdam.

https://p.dw.com/p/4moEK
Mashabiki wa timu ya Maccabi Tel Aviv wakiandamana huko Amsterdam
Mashabiki wa timu ya Maccabi Tel Aviv wakiandamana huko AmsterdamPicha: Mouneb Taim/Anadolu/picture alliance

Viongozi wa Ulaya wameungana na Israel na Uholanzi kulaani vurugu zilizoibuka baada ya mechi kati ya timu za Maccabi Tel Aviv na Ajax ya Amsterdam.

Rais wa  Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen kupitia ukurasa wake wa X ameandika kuwa amekasirishwa na mashambulizi hayo mabaya dhidi ya Waisrael mjini Amsterdam na kuongeza kuwa chuki dhidi ya Wayahudi haina nafasi barani Ulaya. Soma zaidi: Israel yatuma ndege mbili kuwaokoa raia wake Amsterdam

Kwa upande wake Meya wa mji mkuu wa Uholanzi Amsterdam Femke Halsema amesema:

"Amsterdam inatazama nyuma katika usiku wa kutisha na bado hadi sasa ni kiza. Waandamanaji wenye chuki dhidi ya Wayahudi pamoja na wahalifu waliwashambulia na kuwapiga wageni wa Kiyahudi, Waisraeli katika mji wetu jana usiku.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema umefadhaishwa na machafuko yaliyotokea Amsterdam.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Geneva msemaji wa Umoja huo Jeremy Laurence ameeleza kuwa wameziona ripoti hizo zinazotia wasiwasi na kuongeza kuwa hakuna mtu anayepaswa kubaguliwa au kufanyiwa vurugu kwa misingi ya utaifa, dini, kabila au asili.