Viongozi wa Afrika, Asia wakutana Bandung
22 Aprili 2015Akiufungua mkutano huo siku ya Jumatano, Rais Joko Widodo wa Indonesia alitoa wito wa kuundwa mfumo mpya wa kiuchumi duniani pamoja na mageuzi ndani ya Umoja wa mataifa. Katika hotuba yake fupi Widodo alisema ukosefu wa usawa duniani umesababisha uharibifu mkubwa, wakati Umoja wa Mataifa ukionekana unashindwa kuyatatua matatizo ya dunia.
Halikadhalika alisema hatua za matumizi ya nguvu bila ya kibali cha Umoja wa mMtaifa zinaonyesha kutoujali umoja huo. Rais Widodo akasema kwamba, "kwa hivyo nchi za Asia na Afrika, zinadai mageuzi katika Umoja wa Mataifa ili kuweza kufanya kazi kama chombo cha kimataifa kitakachopigania usawa kwa mataifa yote."
Kuimarisha moyo wa Bandung
Pia alieleza kwamba fikra ya kuwa matatizo ya uchumi wa dunia yatatatuliwa na Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na Benki ya Maendeleo ya Asia haina uzito, panahitajika mfumo mpya wa kiuchumi duniani. "Ninaamini jukwaa hili ni pahala pakutambua na kuimarisha moyo wa BANDUNG, kwa ushirikiano na uwekezaji na manufaa ya pamoja," alisema Rais Widodo.
Mkutano huo wa kilele ulihudhuriwa na nchi 92 wakiwemo viongozi 30 wa dunia, akiwemo mwenyekiti wa bunge la umma wa Korea Kaskazini Kim Jong-nam Rais wa China Xi Jinping na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ambao wote waliwasili katika mji mkuu wa Indonesia Djakarta siku ya Jumanne, walitarajiwa kujiunga na viongozi wa Afrika pamoja na Rais Hassan Rouhani wa Iran kuadhimisha miaka 60 ya mkutano wa Bandung uliofanyika1955 na kuundwa Jumuiya ya nchi zisizofungamana na upande wowote wakati ule wa enzi ya vita baridi.
Mkutano ulitarajiwa kufunguliwa na Rais Joko Widodo wa Indonesia, kama sehemu ya siku tano za matukio mbali mbali. Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe, pia alitarajiwa kuhutubia Jumatano, hotuba inayofuatiliwa kwa makini kwa mtazamo wa kumbukumbu ya miaka 70 ya vita vya kwanza vya duniani baadae mwaka huu.
Miaka 60 ya Bandung
Mkutano wa kwanza wa Bandung katika kisiwa cha Indonesia cha Java, ulifunguliwa na shujaa wa uhuru wa taifa hilo Ahmed Sukarno, na ulihudhuriwa na nchi 30, nyingi zikiwa ndiyo kwanza zimepata Uhuru wakati ule baada ya miongo mingi ya utawala wa kikoloni na uvamizi wa wageni.
Viongozi wengine mashuhuri walikuwa Waziri Mkuu wa India Jawaharlal Nehru, Rais wa Misri Gamal Abdel Nasser wakiwa waanzilishi wa jumuiya ya nchi zisizofungamana na upande wowote iliotaka kutojihusisha katika vita baridi si upande wa Marekani wala Muungano wa Jamhuri za Kisovieti yaani Urusi ya zamani.
Mgogoro wa Yemen huenda ukajitokeza
Hata hivyo Jumuiya hiyo imekuwa ikijaribu kuendelea kuwepo hata baada ya vita baridi, huku China ikifanya kampeni kubwa ya kidiplomasia kuwa na ushirikiano wa karibu na bara la Afrika, ambalo mali zake za asili zinasaidia katika ukuaji wa kiuchumi wa dola hilo lenye nguvu kiuchumi barani Asia.
Huenda mgogoro wa Yemen ukaugubika mkutano huo wa Djakarta wakati wanachama wengi wa Jumuiya ya ushirikiano ya nchi za Kiislamu kama vile Iran ambayo inawaunga mkono wanamgambo wa Huthi katika mgogoro huo, wanaweza wakakutana kando kulizungumzia suala hilo.
Wengi wa viongozi katika mkutano huo wa kilele ni kutoka Asia au Afrika, lakini pia kuna wengine kutoka Mashariki ya Kati. Kuna viongozi muhimu kama Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ambaye nchi yake ni mwanzilishi wa Jumuiya ya nchi zisizofungamana na upande wowote na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini hawatahudhuria.
Zuma alivunja safari na kuamua kubakia nyumbani, kutokana na wimbi la mashambulizi nchini mwake dhidi ya wageni kutoka nchi nyengine za kiafrika, wakiwemo kutoka nchi jirani za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,ap.afp
Mhariri:Yusuf Saumu