Viongozi wa Afrika wakutana kujadili masuala ya mazingira
4 Septemba 2023Viongozi hao pia watatowa mwito wa msaada wa kifedha wa kimataifa kusaidia kuimarisha uwezo wake.
Akiufungua mkutano huo,Rais wa Kenya William Ruto amesema anataka mkutano huo wa kwanza wa kilele wa mazingira wa Afrika kusaidia kutowa suluhisho la mtazamo wa waafrika, katika mkutano mkuu wa kilele wa COP28 utakaofanyika mwezi Novemba katika Umoja wa Falme za kiarabu.
"Rafiki zangu ni wakati wa kufikiria mustakabali wa Afrika kwa ujasiri na uthabiti."
Alisema na kuongeza kwamba mkutano huo ni fursa ya kulitazama bara ambalo linaunganisha masoko na rasilimali zenye kuhitajika,kufunguwa uchumi wenye viwango vikubwa.
Soma pia:Papa Francis aionya Mongolia kuhusu rushwa na uharibifu wa mazingira
Aliongeza kwamba "bara ambalo linatowa msingi wa kutengeneza dunia isiyokuwa na hewa chafu."
Ruto aliongeza kwamba mkutano huo unawapa fursa viongozi wa mashirika ya mazingira, wakuu wa nchi fursa ya kufikiria kwa pamoja kuwa na bara ambalo linastawi na kuweka uthibitisho wa mustakali wa kimazingira kwa kila mmoja.
Wachambuzi wanasema ikiwa mkutano wa Nairobi utaweza kuwaleta pamoja viongozi wa bara hilo nakuweka mtazamo wa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nishati mbadala kwa bara hilo, basi hatua hiyo inaweza kuwa chachu ya kuonekana wimbi la mikutano ya kidiplomasia na kiuchumi ya kimataifa kuelekea mkutano wa COP28 huko Dubai.