Viongozi wa BRICS wakutana Durban
27 Machi 2013Bado lakini kuna baadhi ya vizingiti vinavyobidi kuondolewa kabla ya viongozi wa BRICS kutangaza rasmi kuundwa benki hiyo ya maendeleo ya nchi zinazoinukia.Duru za kuaminika zinasema wawakilishi wa Brazil,Urusi,India,China na Afrika Kusini wameshindwa kukubaliana jana usiku kuhusu namna ya kugharimiwa benki hiyo ya maendeleo na wapi yawepo makao makuu yake.Kitita cha Euro bilioni 50 zinahitajika ili kuanza kufanyakazi benki hiyo."Maendeleo ya maana yameweza kupatikana lakini bado uamuzi haujapitishwa kuhusu kuundwa benki hiyo " alisema waziri wa fedha wa Urusi Anton Silouanov jana usiku baada ya mkutano pamoja na mawaziri wenzake,kabla ya mkutano wa kilele unaoanza hii leo.
Waziri mwenzake wa Afrika Kusini Pravin Gordhan ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP,"maendeleo makubwa yamepatikana na kwamba viongozi ndio watakaotoa ufafanuzi wa mpango huo.
Kwa pamoja mataifa ya BRICS yanadhamaini asili mia 25 ya uchumi wa dunia na asili mia 40 ya wakaazi jumla wa dunia.Mvutano unatokana na jinsi ya kugawana mzigo huo wa fedha;baadhi wanahoji kila mwanachama achangie Euro biloni kumi wengine wanataka hali ya kiuchumi ya kila nchi izingatiwe.
Wezani sawa na wa haki
Wanachama wa BRICS wanahisi taasisi mfano wa Benki kuu ya dunia,shirika la fedha la kimataifa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa hazibadiliki kwa haraka kuweza kuambatana na hali namna ilivyo katika nchi hizo.
"Tunashuhudia mwanzo wa enzi mpya zinazotokana na kuchipuka masoko na mataifa yanayonyanyukia kiuchumi"amesema rais Jacob Zuma katika karamu ya ufunguzi wa mkutano wa kilele.
Amesema "BRICS ni mfano mzuri wa utaratibu wa haki wa uongozi".
Benki kuu ya dunia imesema iko tayari kuunga mkono benki hiyo mpya ya maendeleo.
Viongozi wa BRICS wanatarajiwa pia kufikia makubaliano kuhusu kuanzishwa utaratibu wa kubadilisha sarafu ili kurahisisha biashara ya pamoja inayokadiriwa kufikia Euro bilioni 100.
Mbali na mpango huo wa kuunda benki ya maendeleo,viongozi wa BRICS wanatazamiwa kuzingatia wito wa rais Bashar al Assad anaewasihi viongozi hao wapatanishe katika mzozo unaoikaba nchi yake.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu