Viongozi wa dunia wajadili uchumi Davos
22 Januari 2014Pamoja na kasi ya kufufuka kwa uchumi wa dunia, mkutano huo unatarajiwa kujadili namna ya kushughulikia matatizo yanayoendelea kujitokeza kama vile kuzidi kukosekana kwa usawa, ukosefu wa ajira kwa vijana na jamii zinazozidi kuzeeka.
Saa chache kabla ya mkutano huo kuanza, kiongozi wa kanisa katoliki duniani, papa Francis wa pili, aliwatolewa wito washiriki kupunguza umaskini na kuzingatia mahitaji ya makundi yaliyokosa fursa duniani. Papa Francis aliwaomba washiriki hao wahakikishe kuwa binaadamu anahudumiwa na utajiri na si kutawaliwa nao.
Shirika la fedha duniani IMF lilisema jana kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 3.7 mwaka huu, huku likionya juu ya mfumuko mdogo wa bei katika mataifa tajiri na kupanda kwa bei za vitu katika masoko yanayoinukia.
Mabadiliko ya sasa ya dunia
Mwanzilishi wa jukwaa la Davos, Mjerumani Klaus Schwab alisema mkutano wa sasa utajikita katika mabadiliko yanayotokea duniani hivi sasa. "Tukitizama programu za miaka iliyopita, zote zimegubikwa na migogoro, mwaka uliyopita hasa uligubikwa na mgogoro wa kanda inayotumia sarafu ya euro. Sasa ni wakati wa kuangalia mabadiliko makubwa, ambayo yanatokea duniani," alisema Schwab.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na suala la mabadiliko ya tabianchi ambalo viongozi wamesema watalipa umuhimu wa kipekee ili kuunda upya mfumo wa uchumi wa dunia na kupunguza joto la dunia kwa kuhamia vyanzo visafi zaidi vya nishati.
Mkuu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa Chrisitine Figueres, amesema uchumi wa dunia uko hatarini ikiwa mataifa hayatakubaliana kupunguza viwango vya hewa ya ukaa inayotokana na makaa ya mawe na mafuta katika mkutano wa mazingira utakaofanyika mjini Paris mwaka 2015.
Rais wa Korea Kusini Park Guen-hye ameuambia mkutano huo kuwa dunia inapaswa kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kimazingira.
Wakati huo huo, watalaamu wameonya kuwa uchumi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya hautafufuka ipasavyo, ikiwa kanda hiyo haitashghulikia masuala kadhaa ya kijamii, kama vile ukosefu wa ajira.
Mwenyekiti wa benki ya UBS ya nchini Uswisi Axel Weber ameonya kuwa viwango vidogo vya upatikanaji wa ajira vinaweza kuviimarisha vyama vinavyoupinga Umoja wa Ulaya katika uchaguzi wa bunge la Ulaya mwezi Machi, na hivyo kudhoofisha juhudi za kutunga sera mpya za kanda hiyo.
Siasa yatawala mazungumzo
Licha ya jina lake, mkutano huo unajadali zaidi masuala ya kisiasa kuliko uchumi. Mazungumzo ya amani ya Syria yaliyoanza hii leo mjini Montreux na mgogoro wa nyuklia wa Iran vinatarajiwa kuchukua nafasi katika mkutano huo.
Rais wa Iran Hassan Rouhan alitarajiwa kuwasili kwa ajili ya mkutano huo baadae leo, na yeye pamoja na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamepangiwa kutoa hotuba kesho Alhamisi.
Washiriki kadhaa wa Mkutano wa amani ya Syria unaoendelea mjini Montreux, akiwemo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, wametangaza kuwa watakwenda Davos.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe,ape.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo