1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EAC wakutana Dar es Salaam

Mjahida13 Mei 2015

Waandaaji maandamano Burundi wamewahimiza viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaokutana nchini Tanzania kumtaka rais Pierre Nkurunziza kuachia azma yake ya kugombea urais kwa muhula wa tatu.

https://p.dw.com/p/1FP57
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre NkurunzizaPicha: picture alliance/landov

Viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameandaa mkutano wa dharura mjini Dar es Salaam kujadili hali halisi nchini Burundi na kujaribu kutafuta suluhu ya kumaliza maandamano, yaliodumu kwa takriban wiki tatu nchini humo ya kupinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kuwania kipindi cha tatu madarakani.

Kwa sasa takriban watu 20 wameuwawa huku wengine wengi wakijeruhiwa tangu katikati ya mwezi wa Aprili wakati chama tawala cha CNDD FDD kilipomuidhinisha Nkurunziza kama mgombea wao wa Urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi Juni.

Mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama nchini humo yamezua wasiwasi kwamba huenda ghasia zikatokea tena katika nchi hiyo ya Afrika ya kati ambayo bado inajikwamua kutoka miaka kumi na mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka wa 2005.

Raia wa Burundi wakati wa ghasia wa kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu
Raia wa Burundi wakati wa ghasia wa kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatuPicha: Reuters/G. Tomasevic

Aidha rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila, Makamu wa rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na mwanadiplomasia wa Marekani kwa Afrika Linda Thomas-Greenfield pia wanahudhuria mkutano huo wa viongozi wa jumuiya ya EAC, inayojumuisha Kenya, Rwanda, Tanzania, Uganda pamoja na Burundi.

Raia wa Burundi wakimbilia nchi jirani kwa kuhofia usalama wao Burundi

Lakini huku viongozi hao wakitafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Burundi raia wa nchi hiyo takriban 50,000 wameripotiwa kuitoroka nchi hiyo na kukimbilia nchi jirani tangu kuanza kwa machafuko. Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limesema hali ya wakimbizi inazidi kuwa mbaya na huenda wakimbizi hadi 300,000 wakaihama nchi hiyo.

Wakimbizi wanaotokea Burundi wanaosubiri kupokewa nchini Tanzania
Wakimbizi wanaotokea Burundi wanaosubiri kupokewa nchini TanzaniaPicha: DW/P. Kwigize

Wakati huo huo wapinzani nchini Burundi wanazidi kusisitiza kuwa hatua ya Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu madarakani ni kinyume cha katiba.

"Tunatarajia viongozi hao wamwambia rais Nkurunziza kuwa katiba ya Burundi na makubaliano ya amani ya Arusha hayamruhusu yeye kuwania muhula wa tatu," alisema Pacifique Nininahazwe, mwanaharakati na kiongozi wa maandamano ya kupinga hatua ya rais Nkurunziza. Katiba ya Burundi inatoa vipindi viwili tu kwa rais aliye madarakani, na rais Nkurunziza anakaribia kumaliza kipindi chake cha pili kama rais wa nchi hiyo.

Mwandishi Amina AbubakarReuters/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba