1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EAC wakutana kujadili usalama wa Kongo

Thelma Mwadzaya20 Juni 2022

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana jijini Nairobi kujadili hali ya usalama kwenye eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4Cx8S
Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame

Kongo ilijiunga na jumuiya ya EAC mwezi Aprili mwaka huu.Mapigano makali yamekuwa yakiendelea mashariki ya Kongo huku Kigali na Kinshasa wakirushiana vidole vya lawama. Kikao hicho cha faragha ni cha tatu kujadili suala la usalama wa Kongo iliyogubikwa na mapigano kwenye eneo lake la Mashariki.

Kwa mara ya kwanza tangu Rwanda na Kongo kuanza kulaumiana mintarafu waasi wa M23, Rais Paul Kagame amekutana ana kwa ana na mwenzake Felix Tshisekedi kwenye kikao cha Ikulu ya Nairobi.

Baadhi ya viongozi wa EAC wajadili usalama wa Congo, Nairobi

Viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo wa usalama ni Yoweri Museveni wa Uganda, wa Burundi Evariste Ndayishimiye na Salva Kiir wa Sudan Kusini. Tanzania inawakilishwa na balozi wake nchini Kenya John Stephen Simbachawene.

Waasi wa M23 wamekuwa wakiivuruga amani ya mashariki ya Kongo huku serikali kuu ikiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono. Kwa upande wake Rwanda inaendelea kuyakanusha madai hayo.

Ifahamike kuwaJumuiya ya Afrika Masharikiiliunda jopo maalum la usuluhishi linaloegemea zaidi harakati za kukaa kwenye meza ya mazungumzo kati ya waasi na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Jopo hilo linawaleta pamoja wawakilishi wa Kongo, Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya iliyo mwenyekiti wa jumuiya.

EAC Staaten Video-Konferenz
Kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mapema mwaka 2022Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Kwenye taarifa yake, Rais Uhuru Kenyatta alielezea kutamaushwa na hali ya raia wa Kongo wanaohangaishwa na vita. Jumatano iliyopita, mwenyekiti wa Jumuiya ya EAC alitoa wito wa kupelekwa kikosi maalum cha kulinda amani mashariki ya Kongo.

Ili kulitimiza agizo hilo,makamanda wa kijeshi wa Afrika Mashariki waliotakiwa kukutana siku ya Jumapili wanaendelea na maandalizi ya kikosi hicho cha pamoja,EASF.

Kwenye kikao chao cha mwanzoni mwa Juni, Makamanda wa Afrika Mashariki walikutana Goma na kuelezea hatua walizopiga. Jenerali Robert Kibochi ndiye mwenyekiti wa kamati ya makamanda wa EAC na kamanda wa kikosi cha nchi kavu cha Kenya, KDF.

Kufikia sasa, Uganda na Burundi ndio walioonyesha utayari wa kushiriki kwenye juhudi hizo. Kikosi hicho kinatazamiwa kushirikiana kwa karibu na kile cha Umoja wa Mataifa, MONUSCO. Mashariki ya Kongo imevurugwa na mapigano tangu mwishoni mwa Mei.