Viongozi wa NATO kujadili msaada zaidi kwa Ukraine
9 Julai 2024Pia mkutano huo utagubikwa na suala la rais Joe Biden kupambania uhai wake wa kisiasa.
Kiongozi huyo wa Marekani anatarajiwa kutumia mkutano huo wa siku tatu wa maadhimisho ya miaka 75 tangu ulipoanzishwa mfungamano huo wa kiulinzi,kuwahakikishia washirika wake juu ya uongozi wa Marekani na uwezo wake wa kuliongoza taifa hilo, wakati miito ikiongezeka ya kumtaka ajiondowe kwenye kinya'ng'anyiro cha kuwania muhula wa pili madarakani.
Soma pia:Mkutano wa kilele wa Ukraine waanza Uswisi lakini huenda ukashindwa kuitenga Urusi
Hata hivyo viongozi wa NATO wanatarajiwa kuonesha bado wanatambuwa hali halisi inayoendelea katika uwanja wa vita nchini Ukraine.
Rais Volodymyr Zelensky nae pia atashiriki mkutano huo wa Washington akiwa na matumani ya kupata msaada wa mifumo zaidi ya ulinzi wa anga aina ya Patriot ambayo, kwa miezi kadhaa amekuwa akiiomba kwa washirika wake.