Viongozi wa EU wahimiza kuchukuliwa hatua za kuzuia uhamiaji
30 Septemba 2023Waziri Mkuu wa Italia mwenye kuegemea siasa za mrengo mkali wa kulia Giorgia Meloni amesema nchi ziliko kwenye mstari wa mbele zinakabiliwa na idadi kubwa ya wahamiaji, japo bila ya suluhu ya "kimuundo" kutoka Umoja huo, basi kila nchí italemewa.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa wito wa "mwitikio wa pamoja wa Umoja wa Ulaya" akihimiza mshikamano na Italia na nchi zote ambazo huwa za kwanza kupokea wahamiaji.
Soma pia:Wahamiaji 46 na miili kadhaa yapatikana Mediterrania
Viongozi wa nchi zinazojulikana kama "Med 9" walikutana nchini Malta kujadili juu ya kadhia ya wahamiaji, siku moja baada ya mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuafikiana juu ya hatua mpya za kushughulikia suala la wahamiaji.
Kwa jumla, watu wapatao 186,000 waliwasili kwa njia ya bahari kusini mwa Ulaya kuanzia Januari hadi Septemba 24, katika nchi za Italia, Ugiriki, Cyprus, Malta na Uhispania.
Zaidi ya watu 130,000, waliingia Italia - idadi hiyo ikiashiria ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.