1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yawaachia viongozi wa upinzani Tanzania

13 Agosti 2024

Viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, wameachiwa kwa dhamana baada ya kukamatwa kuelekea maandamano ya vijana yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini humo.

https://p.dw.com/p/4jQFe
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema Freeman MbowePicha: Ericky Boniphace/DW

Haya yamesemwa na msemaji wa chama hicho John Mrema. Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, Mrema amesema mwenyekiti Freeman Mbowe na makamu wake Tundu Lissu, wameachiwa na wamerejeshwa Dar es Salaam na maafisa wa polisi na wametoa dhamana.

Msemaji huyo wa Chadema lakini amesema kuna ripoti kwamba baadhi ya viongozi wa tawi la vijana la Chadema, Bavicha, waliokuwa wamekamatwa, bado wanaendelea kushikiliwa na maafisa wa polisi mjini Mbeya.

Taarifa ya polisi ilisema watu 520 walio na mafungamano na chama hicho, wakiwemo viongozi na wanachama vijana, walikamatwa kuelekea mkutano huo wa siku ya vijana uliokuwa umepigwa marufuku.

Lakini imeandika kupitia mtandao wa X, siku ya Jumanne kwamba ofisi zake za Mbeya "zimezingirwa na polisi na hawaruhusu watu kuingia ofisini".

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wapinzani wa serikali yameibua hofu kuwa hatua ya polisi inaweza kuashiria kurejea kwa sera dhalimu za rais wa zamani wa nchi hiyo hayati John Magufuli.

Kukamatwa kwa watu hao kumekuja licha ya mrithi wake Rais Samia Suluhu Hassan kuapa kurejea katika "siasa za ushindani" na kupunguza baadhi ya vikwazo kwa upinzani na vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kuondoa marufuku ya miaka sita ya mikusanyiko ya upinzani.

Chadema yalaani kukamatwa viongozi wake wakuu

Kauli ya polisi

Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi la Polisi Tanzania Awadh Haji, alisema "viongozi wote wakuu wa Chadema waliokamatwa baada ya kuhojiwa na taratibu nyingine wamerudishwa walikotoka”. Haji ameonya kwamba polisi "watachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote au kikundi chochote kinachohusika katika kuvuruga amani".

Ameongeza kuwa maafisa wataendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo na "wataimarisha ulinzi katika jiji la Mbeya na mikoa mingine yote ya Tanzania ili kuzuia vitendo vyovyote vya vurugu vinavyopangwa”.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, alitiwa mbaroni siku ya Jumatatu kwenye uwanja wa ndege jijini Mbeya, siku moja baada ya viongozi wengine kadhaa akiwemo Lissu kuwekwa kizuizini.

Siasa za Chadema: Je, dau la CHADEMA huko Tanzania linayumba?

Mamia ya wafuasi vijana pia walikamatwa na polisi walipokuwa wakisafiri kuelekea mjini Mbeya, kulingana na chama. Takriban watu 10,000 walitarajiwa kukutana jijini Mbeya kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana hapo Jumatatu.

Lakini polisi waliishutumu Chadema kwa kupanga maandamano yenye vurugu na wakirejelea maandamano makubwa ya kuipinga serikali katika nchi jirani ya Kenya, yakiongozwa kwa kiasi kikubwa na wanaharakati vijana.