1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi waafrika washutumiwa kwa kuikataa ICC

21 Januari 2010

Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadam la Human Right Watch leo limetoa taarifa yake ya mwaka ambapo limeangazia masuala mbalimbali ya kukiukwa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/Lcng
Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu

Katika taarifa yake hiyo yenye kurasa mia sita, shirika hilo la Human Right Watch limesema kuwa  hatua ya viongozi wa kiafrika kumuunga mkono Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, kuupinga waranti wa kukamatwa kwake uliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya The Hague, ni kuzuia haki na sheria kuchukua mkondo wake, na kwamba vitisho dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu vimekuwa vikiongezeka.

Kiongozi huyo wa Sudan anatuhumiwa kuhusika na mauaji pamoja na uhalifu wa kivita katika mzozo wa Darfur ambapo zaidi ya watu laki mbili wamekwishauwa na wengine maelfu kadhaa hawana makaazi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo la Human Right Watch, Keneth Roth,ameelezea masikitiko yake kuhusiana na viongozi hao kushindwa kuiunga mkono mahakama ya The Hague juu ya suala la Rais Bashir

Ken Roth präsentiert den Human Rights Watch World Report 2009
Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch, Ken RothPicha: AP
´´Mtu angetegemea kuwa viongozi wa Afrika wangeifurahia waranti hiyo ya kukamatwa Rais Bashir, kuwa hatimaye kuna chombo cha kimataifa ambacho kinatilia maanani wahanga barani Afrika. Lakini bahati mbaya, idadi kubwa ya viongozi wa kiafrika wameamua kumuunga mkono Bashir na siyo wahanga wa vita katika eneo la Darfur. Na wakiongozwa na Libya, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Afrika, Umoja wa Afrika ilitangaza wazi kutoshirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya The Hague katika juhudi za kutaka kukamatwa Bashir. Hii inakatisha sana tamaa´´

Ripoti hiyo  pia imeshutumu unyanyasaji mkubwa wanaofanyiwa wanaharakati wa haki za binaadamu kote duniani, ambapo miongoni mwa nchi zilizotajwa ni pamoja na Kenya, Burundi na Somalia, huku ikisema nchini Sudan kama ilivyo China makundi ya kutetea haki za binaadamu ni kama yamezuiwa kabisa.

Aidha, Human Right Watch imeushutumu utawala wa rais Barack Obama kuwa pamoja na kuahidi kulifunga jela la Guantanamo Bay, na kumaliza utesaji, lakini bado serikali hiyo imekuwa ikitumia njia za kijeshi  kwa baadhi ya washukiwa wa ugaidi.

Kuhusiana na hali katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ripoti hiyo ya shirika la kutetea haki za binaadamu imesema kuwa majeshi ya serikali ya nchi hiyo pamoja na waasi wanawajibika na ongezeko kubwa la vitendo vya uyanyasaji na mauaji dhidi ya raia.

Limesema kuwa takriban raia 2,500 walichinjwa, na wanawake pamoja na  wasichana zaidi ya elfu saba walibakwa, huku wengine zaidi ya millioni moja wakiyakimbia makaazi yao.

Shirika hilo limeionyooshea kidole serikali ya Kenya kwa kushindwa kufanya mabadiliko, kama ambavyo jumuiya ya kimataifa ilipendekeza, kufuatia ghasia kubwa zilizosabishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.

Shirika hilo limesema kuwa ripoti yake hiyo ya mwaka kuhusiana na masuala mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binaadamu duniani, ni katika kumkumbuka aliyekuwa afisa mwandamizi wa shirika hilo kwa Afrika na ambaye alikuwa mtaalam wa mauaji ya halaiki ya Rwanda ya mwaka 1994, Alison Des Forges, aliyefariki katika ajali ya ndege mwaka jana nchini Marekani.

Mwandishi.Aboubakary Liongo/HRW/Reuters

Mhariri:Othman Miradji