1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wajadili mkataba wa taka za plastiki

23 Aprili 2024

Viongozi wa kimataifa wamekusanyika katika mji wa Ottawa nchini Kanada kwa mazungumzo ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na uchafuzi wa plastiki duniani.

https://p.dw.com/p/4f6RD
Uchafuzi wa taka za plastiki
Taka za plastiki zikivuliwa kutoka katika mto Gitadhuru Nairobi KenyaPicha: Gerald Anderson/AA/picture alliance

Mkataba huu ulitarajiwa kufikiwa mwishoni mwa mwaka uliopita, lakini mazungumzo yakasogezwa mbele. Mjini Ottawa wapatanishi katika mazungumzo haya wanakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutokana na mgawanyiko miongoni mwa nchi wanachama juu ya jinsi mkataba huo unavyopaswa kutekelezwa.

Kulingana na afisa wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa

Jyoti Mathur-Filipp mazungumzo haya ni muhimu, akiyataja kama fursa ya kupiga hatua kuelekea makubaliano thabiti ambayo yataruhusu vizazi vijavyo kuishi katika ulimwengu usio na uchafuzi wa plastiki.

Wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 170 wanatarajiwa kushiriki.

Shinikizo linaongezeka kwa wajumbe kufikia rasimu ya makubaliano kabla ya duru ya mwisho ya mazungumzo kufanyika nchini Korea Kusini mwezi Disemba.

Soma pia: Mazungumzo ya kudhibiti plastiki yakumbwa na kutoelewana

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliweka azma ya kuafikiana juu ya mkataba wa kimataifa ifikapo mwisho wa mwaka huu. Lakini mkutano wa awali uliofanyika Kenya mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita haukupata mafanikio makubwa.

Kulingana na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, kila siku, kiasi cha tani 2,000 za takataka zilizojaa plastiki hutupwa kwenye bahari, mito na maziwa duniani. Na kwamba watu wanazidi kupumua, kula na kunywa chembe ndogo za plastiki.

Soma pia: Kizazi cha mwisho waitisha maandamano ya tabianchi Ujerumani

Athari za taka za plastiki

Mazungumzo ya makubaliano ya plastiki.Paris
Mkutano wa mazungumzo yamakubaliano mapya ya kimataifa ya plastiki huko Paris, Ufaransa.Picha: Stephanie Lecocq/REUTERS

Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira unaozijumuisha Japan na Umoja wa Ulaya umetuma wajumbe wake katika mkutano huu ukihimiza nchi zinazojadili mkataba huo kujumuisha wasiwasi kuhusu athari za plastiki kwa viumbe hai, iwe ni mimea au wanyama.

Mshauri Mkuu wa Sera wa  muungano huo, Dkt Karine Siegwart, anasema kupuuza athari za plastiki kwa asili sio chaguo kwa nchi yoyote kwani kila mfumo wa ikolojia unaathiriwa

"Plastiki sasa iko kila mahali, iko kwenye maji yetu safi, iko kwenye mito na maziwa. Tunapata chembechembe za plastiki kwenye kila ziwa, milimani, ardhini na hewani.

"Plastiki iko kila mahali, na iko katika miili ya wanadamu na viumbe vyengine na mifumo ikolojia huathiriwa sana."

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban tani bilioni 9.2 za plastiki zimezalishwa tangu mwaka 1950 huku idadi kubwa ya taka hizo zikiwa haziwezi kuoza na hivyo kuishia kurundikana baharini na mitaani.