Viongozi waungane kumaliza changamoto za usalama Afrika.
17 Julai 2023Mkutano mkubwa wa mwaka unaoangazia masuala ya uongozi na demokrasia na uliowashirikisha marais watatu wastaafu wa nchi za Afrika, pamoja na mambo mengine umesema demokrasia katika bara hilo ipo mashakani.
Katika mkutano huo, wakuu hao wa nchi wastaafu pamoja na kueleza baadhi ya mafanikio ambayo nchi nyingi za Afrika zimefikia baada ya uhuru lakini wamekosoa mienendo ya utawalawa baadhi ya serikali za Afrika kwamba haizingatii utawala wa kisheria, demokrasia na ulinzi wa raia.
Rais mstaafu wa Sierra Leone aliyeiongoza nchi hiyo kati yam waka 2007 hadi 2018, pamoja na mambo mengine amebainisha kwamba demokrasia Afrika inakuwa mashakan kutokana na kushuhudiwa matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu na usalama wa raia.
Soma Pia:Mapigano yazuka tena Rutshuru kati ya M23 na Mai Mai
Akitolea mfano baadhi ya vyanzo vinavyoweka democrasia rehani ni pamoja na matukio ya chaguzi zisizozingatia sheria, kunyamazishwa kwa vyama vya upinzani na mamlaka za dola kuwaonea raia badala ya kuwalinda.
Alisema kuna baadhi ya mambo mengi yanatokea Afrika na kuwaacha watu wetu na maswali mengi yasiyo na majibu.
"Vita vinavyoendelea Sudan, Migogoro ya kiusalama Somali, Nigeria, Mali na jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kwingineko ni mifano tu ya matukio mengi."
Alisema rais huyo mstaafu na kuongeza kwamba njaa ,vita , umaskini na athari za mabadiliko ya tabia nchi, zinawafanya raia wengi kujihisi wametengwa.”
Tanzania yapongezwa kupiga hatua kwenye democrasia?
Rais mstaafu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete pamoja na kugusia baadhi ya changamoto za kidemokrasia zinazozikabili baadhi ya nchi za Afrika, ameipongeza Tanzania kwa madai kwamba imepiga hatua nzuri katika hilo mpaka sasa, ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita.
"Ni taifa tunalojivunia la watu milioni 61 lililo na makabila tofauti, dini pamoja na vyama vingi vya siasa."
Alisema Jakaya Kikwete na kutilia mkazo kwamba licha ya taifa hilo la Afrika Mashariki kuwa na idadi kubwa ya makabila bado watu wake wanasikilizana na kuamua kwa pamoja masuala ya ndani.
Soma Pia:Mashirika ya haki za binadamu yatoa wito wa majadiliano Tanzania
Awali akifungua mkutano huo Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambae ni mwenyeji, katika hotuba yake alinukuu takwimu zinazoonesha kwamba nchi 25 kati ya 54 za Afrika zimekabiliwa na mizozo ya kisiasa inayotokana na katiba tangu mwaka 2010.
Kulingana na ripoti ya kituo cha kimataifa cha taarifa za uchunguzi, Afrika haijawa salama kwa miaka minane iliyopita kutokana na migogoro inayoendelea katika nchi mbalimbali ikiwepo Sudan na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
Akitolea mfano ndani ya taifa lake ambalo lilipitia pandashuka chungumzima chini ya mtangulizi wake hayati John Pombe Magufuli ambae kwa kiwango kikubwa alishutumiwa na jumuiya za kimataifa na upinzani kwa kundamiza vyama vya upinzani na wakosoaji wake.
Alisema kwamba Tanzania imechukua hatua kadhaa za kuimarisha demokrasia hasa katika autawala wake, ikiwemo kuleta maridhiano ya kitaifa.
"Ajenda ya maridhiano tuliifanya na vyama vya upinzani na wadau wengine."
Tumefanikiwa kuondoa tofauti zetu. Tunaweza kupishana kidogo lakini sio kwa kiwango cha kuvuruga amani ya nchi.”
Baadi ya wakuu wan chi waliohudhuria mkutano wa leo ni pamoja na Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma.
Hata hivyo Rais mstaafu Joaquim Chissano Msumbiji akitarajiwa kuungana na wenzake pamoja na wadau wengine kushiriki mkutano unaofutia wa siku mbili utakaojadili mustakabali wa demokrasia barani Afrika.