Utafiti huo mpya ambao umechunguza ajali za barabarani tangu Januari 2021 hadi mwezi Septemba unaonesha wakenya 3200 walikufa ndani ya kipindi cha miezi tisa pekee.
Hizo ni takwimu za kutisha kwa sababu, tofauti na mwaka uliopita, wakenya 700 zaidi wamekufa mwaka huu kutokana na ajali za barabarani.
Ripoti hiyo inasema miongoni mwa walioaga dunia mwaka huu, watu 1,100 ni wanatembea kwa miguu, madereva 300, abiria 318, waendesha boda boda 890 na waendeshaji baiskeli 61.
Ripoti hiyo inasema kuwa baadhi ya ajali hizo zimetokana na madereva kutozingatia sheria za barabarani, kasi kupita kiwango, ulevi wa madereva na waendesha pikipiki na baiskeli miongoni mwa mambo mengine. Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Edward Mbugua ananyoshea kidole cha lawama ukosefu wa kuongezeka kwa miundo mbinu.
“Kumekuwa na mamalamiko mengi kuwa kuna ongezeko la ajali, lakini tunajiuliza idadi ya magari yanayoongezeka barabarani kila mwaka? Barabara haziongezeki,” amesema Edward.
Mwaka uliopita katika kipindi kama hiki watu 930 wanaotembea, madereva 210, abiria 330 na bodaboda 740 walipoteza maisha yao kwa ajali. Watu 7,000 walipata majeraha mabaya mwaka huu huku 5000 wakijeruhiwa vibaya mwaka uliopita.
Jumla ya visa 2,820 vya ajali mbaya viliripotiwa katika kipindi cha utafiti huo ikilinganishwa na visa 2,200 mwaka uliopita. Felix Ochieng ni mchambuzi wa masuala ya kijamii, anatupa mtazamo wake.
Kufuatia ongezeko la visa vya ajali, maafisa wakuu wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama nchini Kenya walikutana na uongozi wa polisi kuangazia suala hilo.
Walikubaliana kuongeza kampedni dhidi ya vyanzo vya ajali ambavyo husababisha maafa na kuacha wengi na majeraha.
Mwenyekiti wa NTSA George Njao alisema kuwa watashirikiana na mashirika mengine kuangazia janga hilo.
Hata hivyo mwenyekiti wa Chama cha Usalama Barabarani David Kiarie amelaumu NTSA kwa uzembe ambao umechangia ongezeko la ajali barabarani.
Kipi kifanyike ili kuzuia ongezeko la ajali za barabarani? Swali hilo nilimuuliza Fred Wafula ambaye ni mchambuzi wa masuala ya jamii.
NTSA imesema kuwa itashirikiana na serikali za majimbo kupitia kamati za Usafiri na Usalama kutafuta mbinu za kupunguza ajali za barabarani. Mkakati huo utafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya chini yenye kauli mbiu “Usalama Barabarani”.