1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa vya Ebola vimeongezeka magharibi mwa Afrika

Admin.WagnerD23 Oktoba 2014

Shirika la afya duniani WHO limesema visa vya watu walioambukizwa virusi vya Ebola katika nchi za magharibi mwa Afrika vinatarajiwa kufika 10,000 huku juhudi za kutafuta tiba ya ugonjwa huo hatari zikishika kasi

https://p.dw.com/p/1DaDc
Picha: picture-alliance/dpa/Alex Duval Smith

Shirika la afya duniani limesema watu 9,936 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone nchi ambazo zimeathirika vibaya zaidi na Ebola wameambukizwa ugonjwa huo huku watu 4,877 wakiripotiwa kufariki kufikia sasa.

Huku wataalamu wakionya kuwa kiwango cha maambukizi huenda kikawa watu 10,000 kwa wiki ifikapo Desemba, watafiti kote duniani wanang'angana kutafuta suluhisho la kuudhibiti ugonjwa huo ambao kwa wakati huu hauna tiba au chanjo iliyoidhinishwa rasmi kupambana nao.

WHO inafanya mkutano wa dharura

Takwimu hizo zimetolewa wakati WHO ikifanya mkutano wake wa tatu wa dharura hii leo kuhusu Ebola ili kujadili juhudi za kuudhibiti. Mkutano na wanahabari kuhusu yatakayokuwa yamejadiliwa katika mkutano huo utafanywa hapo kesho baada ya kukamilika kwa mazungumzo.

Naibu Mkurugenzi mkuu wa WHO Marie Paule Kieny
Naibu Mkurugenzi mkuu wa WHO Marie Paule KienyPicha: Getty Images

Wakati huo huo, chanjo ya majiribio ya rVSV dhidi ya Ebola imewasili katika chuo kikuu cha Geneva kutoka Canada.WHO itaratibu majaribio ya chanjo hiyo sambamba na chanjo nyingine zinazofanyiwa majaribio Ujerumani, Gabon na Kenya.

Naibu mkurugenzi mkuu wa WHO Marie Paule Kieny amesema lengo ni kusafirisha chanjo kuelekea Afrika ifikapo mapema mwaka ujao ili kuanzishwa kwa kampeini kubwa ya kutolewa kwa chanjo hiyo ambayo bado haijaorodheshwa katika kadi za chanjo.

Hayo yanakuja huku Marekani ikiimarisha madurufu uchunguzi wa kimatibabu kwa wasafiri wanaotokea nchi za magharibi mwa Afrika zilizoathirika na Ebola na kutangaza wasafiri hao watalazimika kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa siku ishirini na moja.

Rais wa Marekani Barrack Obama amesema kukiwa na mifumo muafaka Ebola inaweza kudhibitiwa kama ilivyokuwa Senegal na Nigeria

Wasafiri walio na jamaa wagonjwa kutosafiri

Na Liberia imeanza kutumia mfumo wa kuwianisha taarifa za jamaa ili kuzuia wasafiri ambao wana jamaa zao waliogua Ebola hata kama hawana dalili za maambukizi kutosafiri nje ya nchi hiyo ili kupunguza kuusambaza ugonjwa huo katika nchi za kigeni.

Raia wa Liberia wakisubiri kuchunguzwa kabla ya kusafiri
Raia wa Liberia wakisubiri kuchunguzwa kabla ya kusafiriPicha: AFP/Getty Images/Z. Dosso

Rwanda nayo imefutilia mbali vikwazo ilivyokuwa imeweka dhidi ya wasafiri kutoka Marekani na Uhispania kama njia mojawapo ya kuzuia Ebola kuingia nchini humo.

Waziri wa afya wa Rwanda Agnes Binagwaho wiki hii aliagiza wasafiri wote kutoka Marekani na Uhispania kuifahamisha wizara yake kila siku kwa wiki tatu ambazo watakuwa nchini humo hali yao ya kiafya baada ya visa vya Ebola pia kuripotiwa katika nchi hizo mbili.

Taarifa kutoka kwa Rais Paul Kagame hata hivyo imesema agizo hilo limefutiliwa mbali kwani haihitajiki na kuongeza waziri huyo saa nyingine huchukua hatua za haraka na kufikiri baadaye badala ya kuwa vinginevyo.

Wasafiri kutoka Guinea,Liberia na Sierra Leone wamezuiwa kuingia Rwanda na raia wake ambao wamesafiri katika nchi hizo tatu wanawekwa karantini kwa siku ishirini wanapowasili.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Yusuf Saumu