Visa vya ubaguzi vimeongezeka Ujerumani
9 Juni 2020Tangu kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd kilichorekodiwa kwenye vidio, maandamano yamefanyika sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Ujerumani.
Watu wengi nchini Ujerumani walishtushwa na vidio ya kifo cha maumivu alichopitia George Floyd baada ya kuwekewa goti na kukandamizwa shingoni kwa takribani dakika tisa na askari polisi mweupe. Maelfu ya watu waliingia mitaani nchini Ujerumani kupinga mauaji hayo licha ya vizuwizi vilivyowekwa kudhibiti mripuko wa ugonjwa wa covid-19.
Katika wakati ambapo kuna nadhari kubwa ya vyombo vya habari, waandamanaji hao wamelalamika juu ya ubaguzi wa rangi nchini Ujerumani. Kwa sababu taswira ya jamii ya Ujerumani pia, imetiwa dosari na ubaguzi wa kila siku, machafuko ya chuki dhidi ya wageni na mashambulizi ya wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia. Takwimu za karibuni zinaunga mkono ukosoaji wa waandamanaji na kuthibitisha mwelekeo wa kusikitisha: Ubaguzi wa rangi umeongezeka nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya 2019 iliyowasilishwa Jumanne na shirikisha la serikali ya Ujerumani linalopambana dhidi ya ubaguzi, ADS, idadi ya visa vya ubaguzi wa rangi vilivyoripotiwa nchini humo iliongezeka kwa asilimia karibu 10 hadi 1,176. Visa hivyo vinachangia asilimia hadi 33 ya visa vinavyoshughulikiwa na wakala huo. Hiyo ndiyo sehemu kubwa zaidi, na siyo kwa mara ya kwanza. Mwaka 2016, ilikuwa asilimia 25. Tangu 2015, wakati visa 545 viliporipotiwa, idadi imeongezeka zaidi ya mara mbili.
Kaimu mkuu wa wakala huo wa ADS Bernard Franke, amesema wakati akiwasilisha ripoti hiyo kwamba Ujerumani ina tatizo linaloendelea la ubaguzi wa rangi na haitoi msaada wa kutosha na endelevu kwa waathirika. Hisia za kuachwa mpweke na dhulma, zina madhara makubwa katika kipindi cha muda mrefu ambayo yanahatarisha mshikamano, ameonya Franke na kuongeza kuwa "ubaguzi unadhoofisha watu."
Watu wenye asili ya uhamiaji wanahisi kutengwa
Kwa sababu hii, ripoti ya kila mwaka ya ADS inajikita juu ya suala la ubaguzi wa rangi kwa mapana na marefu. Katika dibaji ya ripoti hiyo, Franke ameandika kwamba 2019 ulikuwa mwaka ambamo "chuki na uhasama kwa makundi makhsus viliacha mikururo ya maumivu makali" - kuanzia mauaji ya mwanasiasa wa chama cha CDU Walter Lübcke, aliepigania haki za wakimbizi, yaliofanywa na mfuasi wa itikadi kali za mrengo wa kulia - hadi shambulizi la kigaidi dhidi ya sinagogi mjini Halle.
Lakini pia amesema kulikuwepo na matukio mengi madogo na ubaguzi wa kila siku vilivyoacha alama. Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa wengi walioathirika wana hisia kwamba kwa jumla hali haijaboreka katika miaka iliyopita. Wanahisi ingawa mashambulizi na mauaji vimetikisa jamii, wasiwasi, hofu na uzoefu wa kutengwa na watu wenye asili ya uhamiaji havichukuliwi kwa uzito.
Ripoti hiyo inaangazia baadhi ya matukio ya ubaguzi ikiwa ni pamoja watu wenye asili ya kigeni kubaguliwa katika upangishaji wa nyumba, kukataliwa kuingia baadhi ya maeneo na wasimamizi wa kazi kuwatetea watu wanaotoa matamshi ya ubaguzi kwa kusema wanaotoa matamshi hayo hawakudhamiria. Ripoti inazungumzia kwa mfano, utafiti ulioonyesha kuwa asilimia 41 ya wamiliki wa nyumba wana wasiwasi kuhusu kuwapangisha raia wenye asili ya kigeni.
Kimsingi, sheria ya usawa nchini Ujerumani, inakataza vitu kama hivyo, lakini ulinzi jumla dhidi ya ubaguzi wa rangi katika soko la nyumba unaainishwa na mambo ya kipekee kwa mujibu wa ripoti ya ADS. Mtazamo wa kisheria ulioagizwa na wakala huo umehitimisha kwamba muongozo wa Umoja wa Ulaya kuhusu kukabiliana na ubaguzi wa rangi haujatekelezwa ipasavyo nchini Ujerumani.