Vita vya Israel-Hamas: Israel yaanza tena mashambulizi
1 Desemba 2023Dakika chache baada ya saa moja asubuhi ya Ijumaa kwa majira ya Mashariki ya Kati, jeshi la Israel lilisema limeanzisha tena mapigano dhidi ya wanamgambo wa Hamas, kundi ambalo Umoja wa Ulaya pamoja na nchi nyingine ikiwemo Marekani, zimeliorodhesha kuwa la kigaidi.
Israel ilidondosha vijikaratasi vyenye taarifa ya kuwatahadharisha wakaazi wa baadhi ya maeneo ya kusini mwa Gaza kuondoka katika majumba yao, ikiashiria ilikuwa ikijiandaa kutanua operesheni zake.
Moshi mweusi ulionekana ukitanda katika eneo linalozingirwa na Israel kufuatia mashambulizi ya ndege zake za kivita katika baadhi ya maeneo ya Hamas.
Vikosi vya jeshi la Israel IDF vimesema Hamas ilivunja makubaliano ya usitishaji vita kwa kufanya shambulizi kuelekea Israel.
Jeshi hilo la Israel limeongeza kuwa, muda mfupi tu kabla ya makubaliano hayo kukamilika, mifumo yake ya ulinzi ya angani ilizuia roketi inayoshukiwa ilifyatuliwa kutoka Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi mapya yazusha wasiwasi kuhusu mateka waliosalia Gaza
Kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji vita kumejiri siku moja tu baada ya waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kukutana na maafisa wa Israel.
"Katika mkutano wangu leo na Waziri Mkuu na maafisa wa ngazi za juu wa Israel, nilieleza wazi kwamba kabla ya Israel kuanza tena operesheni kubwa za kijeshi, lazima iweke mipango ya ulinzi wa kibinadamu kwa raia, mipango itakayopunguza maafa zaidi ya Wapalestina wasio na hatia," alisema Blinken.
Netanyahu na vita mbili zinazomkabili - Hamas na nyumbani
Blinken alikuwa njiani kuelekea Dubai kwenye mkutano wa mazingira wa COP28, ambapo atafanya mkutano na viongozi wa Kiarabu na wa mataifa mengine pembezoni, kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati.
Mapigano hayo mapya yamezidisha wasiwasi kuhusu takriban mateka 140 ambao bado wamesalia Gaza, baada ya zaidi ya 100 kuachiliwa huru kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji vita.
Awali, Israel na kundi hilo la wanamgambo wa Kiislamu, walikubaliana kusitisha mapigano kwa siku nne kuanzia Novemba 24. Baadaye muda wa makubaliano hayo ulirefushwa hadi Ijumaa asubuhi. Mnamo dakika za mwisho za kukamilika kwa makubaliano hayo, haikuwa imebainika waziwazi ikiwa yangerefushwa tena.
Usitishaji mapigano ungerefushwa hadi siku 10 ikiwa ...
Kulingana na makubaliano ya awali, usitishaji mapigano ungerefushwa hadi siku kumi, ikiwa wanamgambo wa Hamas wangeendelea kuwaachilia huru mateka waliowakamata wakati walipofanya shambulizi baya kusini mwa Israel Oktoba 7, huku Israel, ikiwaachilia baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walioko katika magereza yake.
Israel na Hamas waendelea kubadilishana mateka na wafungwa
Usitishaji huo wa mapigano pia uliwezesha misaada iliyohitajika kupelekwa katika Ukanda wa gaza kwa wahanga wa vita.
Katika shambulizi la kushtukiza la Oktoba 7, lililofanywa na wanamgambo wa Hamas, takriban watu 1,200 waliuawa ndani ya Israel karibu na mpaka wake na Gaza, na takriban watu 240 walishikwa mateka.
Israel ilijibu kwa kutangaza vita dhidi ya Hamas na kuanzisha mashambulizi makali zaidi ya angani katika ukanda huo wa Gaza ulio na idadi kubwa ya watu. Aidha vikosi vya Israel vilianzisha operesheni ya ardhini katika pwani ya Gaza ambapo Hamas ilichukua madaraka yake kwa nguvu mnamo mwaka 2007.
Tangu kuanza kwa vita, takriban watu 15,000 wameuawa Gaza na zaidi ya 36,000 wamejeruhiwa. Hayo ni kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas. Takwimu hizo bado hazijaweza kuthibitishwa na shirika huru.
Bonyeza hapa ufahamu zaidi kuhusu Mzozo wa Israel na Hamas
Vyanzo: DPAE, APAE, EBU