1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Vita vya Israel na Hamas: Idadi ya waliouawa yafikia 9,000

Sylvia Mwehozi
2 Novemba 2023

Vikosi vya Israel vimeendelea kusonga mbele kuingia Gaza City lakini vimekumbana na upinzani mkali kutoka wapiganaji wa Hamas waliowashambulia kwa makombora na mashambulizi ya kushtukiza kutoka kwenye mahandaki.

https://p.dw.com/p/4YKbW
Ukanda wa Gaza
Kifaru cha Israel karibu na mpaka wa GazaPicha: Yuri Cortez/AFP/Getty Images

Ikiwa ni siku ya 27 tangu vita hivyo vianze, wanajeshi wa Israel wanazidi kusogea katika eneo lenye wakaazi wengi katika Ukanda wa Gaza upande wa Kaskazini ambako Israel iliapa kusambaratisha muundo wa kundi hilo la wanamgambo na kuwataka raia kuondoka.

Kamanda wa jeshi la Israel Brigedia Jenerali Itzik Choen amesema jeshi lake "lipo katika milango ya Gaza City." Kwa mujibu wa mashuhuda ni kwamba wapiganaji wa Hamas na washirika wao wa kundi la Islamic Jihad, walikuwa wakitokea kwenye mahandaki na kurusha makombora na kisha kurudi ndani ya mtandao huo wa mahandaki, mithili ya mbinu ya vita vya msituni.

Kwa kufahamu ugumu wa mapigano katika mazingira ya mijini, mkakati wa maafisa wa Israel unaonekana kwa sasa kuelekezwa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza badala ya kuanzisha mashambulizi ya ardhini katika eneo lote.

Kambi ya wakimbizi ya Jabalia
Wapalestina wakikagua vifusi katika jengo lililoharibiwa kambi ya wakimbizi ya JabaliaPicha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Wakati mapambano hayo yakiendelea, wizara ya afya ya Hamas inasema idadi ya watu waliouawa tangu vita vianze imepindukia 9,000 na kati yao 3,760 ni watoto na zaidi ya elfu 32,000 wamejeruhiwa.  

Soma pia pia: Misri yawapokea majeruhi kutoka Ukanda wa Gaza

Umoja wa Falme za Kiarabu umejitolea kuwatibu watoto 1,000 walioandamana na familia, huku Uturuki ikijitolea kuchukua wagonjwa wa saratani kutoka hospitali yenye ushirikiano na Uturuki na Palestina huko Gaza, ambayo ilishindwa kufanya kazi baada ya kukosa mafuta. Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Juliette Touma anasema maji yanakaribia kuisha na usambazaji wake umekuwa ukiingiliwa.

Watu zaidi ya 500 wadaiwa kuuwawa hospitalini Gaza

"Maji yanatumika kama silaha ya vita. Watu wengi wanakimbilia kwenye vyanzo vya maji visivyo salama, kwa mfano tulisikia maji ya baharini, maji ya visima, maji yasiyosafishwa na hiyo ni hatari sana kwa sababu inaweza kuchangia magonjwa ya milipuko kwa  watoto na watu wazima. Kwahiyo, maji safi huko Gaza ama hayapatikani kabisa au yanapatikana kwa kiwango kidogo sana."

Tamko la MSF: MSF: Majeruhi zaidi ya 20,000 bado wamekwama Gaza

Kando na mapigano, Saudi Arabia imetangaza ufadhili mwingine wa Dola milioni 13 kwa ajili ya misaada ya kiutu kwa Wapalestina walioko Gaza, hii ikiwa ni kwa mujibu wa kituo cha msaada wa kibinadamu cha Mfalme Salman. Taarifa hiyo imesema Mfalme Salman na Mwanamfalme Mohammed bin Salman watachangia fedha hizo wao wenyewe. Kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2015 kinafanya kazi na mashirika ya Umoja wa Mataifa katika mataifa zaidi ya 100.

Na wakati huo pia Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamekubaliana juu ya haja ya kuongeza kasi ya usambazaji wa misaada ya kiutu Gaza. Viongozi hao wamekutana katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa usalama wa teknolojia ya akili bunifu huko England.