Vita vya Ukraine vyahatarisha hali ya maisha Yemen na Misri
28 Februari 2022Vita nchini Ukraine huenda vikatishia uhaba wa mikate katika nchi nyingi za Mashariki ya kati ambazo zinategemea ngano kutoka Urusi. Huenda vita hivyo vinafanyika maelfu ya maili lakini huko Yemen kwa watu kama Ilham mwenye umri wa miaka 32 familia yake itayapata maumivu yanayosababishwa na mgogoro huu watakapofika kwenye meza ya chakula.
Mgogoro kati ya Ukraine na Urusi ambazo ni wasambazaji wa zaidi ya robo ya mahitaji ya ngano duniani umeshasababisha gharama ya bidhaa hiyo kupanda. Na hali hiyo imesababisha tahadhari kubwa katika eneo la nchi za Mashariki ya kati ambazo zinategemea ngano kwaajili ya chakula kinacholiwa kila siku kuanzia mkate mpaka CousCous.
Ilham ambaye hakutaka kutajwa jina lake kamili amezungumza na shirika la habari la reuters na kusema kwamba tayari gharama imeongezeka kwahivyo hawezi kujua nini kitatokea wakati bei ya ngano itapanda zaidi. Kwengineko ambako kuna matatizo ya chakula katika eneo hilo wateja wanaonekana kujaribu kununua kwa wingi mikate mapema ili kuepuka bei kubwa wakati waokaji mikate nchini Misri wakisema tayari walikuwa wakishuhudia athari za ongezeko la bei ya unga wa ngano.
Kote Mashariki ya kati na Afrika Kaskazini,kuongezeka gharama ya chakula kutoka na vita vya Ukarine huenda kukasababisha mamilioni ya watu kuingia kwenye umasikini wa kukosa chakula. Hayo yameelezwa na msemaji mwandamizi wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP kanda hiyo Abeer Etefa.
Kanda hiyo kimsingi hasa inakabiliwa na hatari ya kushuhudia ongezeko la bidhaa za vyakula kutokana na ukosefu wa uzalishali chakula ndani pamoja na viwango vikubwa vya umasikini,ambapo hasira zilizosababishwa na gharama kubwa ya bei ya vyakula iliwahi kuchochea maandamano katika nchi nyingi za kiarabu mnamo mwaka 2011.
Yemen ambayo inategemea chakula kutoka nje kwa takribana kila kitu inanunua alau kiasi asilimia 27 ya ngano yake kutoka Ukraine na asilimia 8 kutoka Urusi,kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa masuala ya fedha na muagizaji mkubwa wa ngano nchini humo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Miaka saba ya vita imeuharibu kabisa uchumi wa Yemen na kusababisha ukosefu mkubwa wa ajira na kuongeza mara mbili bei ya vyakula nchini humo na kuacha zaidi ya nusu ya watu wa nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni 30 kukabiliwa na njaa,kulingana na kamati ya kimataifa ya uokozi.
Itakumbukwa kwamba mwaka jana kupungua ufadhili kulilifanya shirika la kimataifa la mpango wa chakula duniani WFP kupunguza msaada wake kwa watu milioni nane wa Yemen na kuiweka hatarini nchi hiyo kutumbukia kwenye janga kubwa la njaa.
Na hivi sasa uwezekano wa kuongezeka zaidi kwa bei ya ngano duniani kunamaanisha Wayemen huenda wakajikuta wako hatarini zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine,amesema Afrah Al-Zouba, ambaye ni mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Yemen linalofanya kazi ya kusaidia upatikanaji wa msaada.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Daniel Gakuba