Vitisho vya rais Trump wa Marekani kwa Iran Magazetini
21 Mei 2019Tunaanza na vitisho vya Marekani dhidi ya Iran. Baada ya Marekani kujitoa katika mkataba wa mradi wa nuklea na kutangaza vikwazo ziada, Iran nayo inasema itarutubisha madini ya urani. Gazeti la "Badische Zeitung" linalinganisha kadhia ya Marekani na Iran na ile ya Korea ya kaskazini na kuandika: "Vita vya maneno vinatukumbusha mvutano kama huu uliokuwepo kati ya Marekani na Korea ya kaskazini, dola hilo linalomiliki silaha za nuklea ambalo Trump alitishia kulihujumu kwa moto ili kulilazimisha lisitishe mradi wake wa nuklea.
Kilichofuatia kingebidi kiwazinduwe vichwa mchungu wa Iran na kutafakari. Licha ya kuitwa "Kibabu cha kombora" Kim Jong-Un alimalizikia kuonekana kuwa kiongozi mwenye busara kwasababu ya kuonana na Trump. Hali hiyo haikubadilisha chochote, na Pyongyang haina fikra hata kidogo ya kuachana na mradi wake wa nuklea.Yalikuwa makelele matupu, angalao hadi sasa."
Madhara ya vikwazo vya Trump kwa wanunuzi
Kama vitisho vya Marekani dhidi ya Iran vitasalia maneno matupu hakuna bado ajuaye, kinachojulikana lakini ni madhara ya hatua za Marekani dhidi ya kampuni la elektroniki la China Huawei. Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linaandika: "Kwa mara nyengine tena rais wa Marekani hajali madhara ya aina gani yanasababishwa na mchezo wake wa kutunisha misuli-si kwa uchumi na wala si kwa wanunuzi. Licha ya kudhihirika kwa mara nyengine tena kwamba katika mfumo unaotatanisha wa uchumi wa dunia, vikwazo na vizingiti vya kibiashara havimuathiri mdau mmoja tu aliyekusudiwa-yanamuathiri kila mtu."
Kashfa ya FPÖ yaitikisa serikali ya kansela kurz
Kashfa iliyopelekea kuvunjika serikali ya muungano nchini Austria inaendelea kugonga vichwa vya habari nchini Ujerumani . Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Mbegu ya mzozo huu wa sasa wa serikali ilioteshwa tangu mwnzo-katika mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano. Kurz aliwaachia FPÖ wizara nne muhimu, ikiwa ni pamoja na wizara ya mambo ya ndani. Kashfa zote na matamshi ya chuki ya FPÖ, kansela Kurz alikuwa akinyamaza au akitoa onyo lakini dhaifu. Hivi sasa na baada ya kusita sita Kurz ameamua hatimae kuvunja moja kwa moja muungano pamoja na FPÖ. Kama uamuzi huo utamsaidia aaminike- hakuna ajuaye bado."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Sekione Kitojo