1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen: Hatma ya Ukraine imo ndani ya Umoja wa Ulaya

13 Septemba 2023

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen ametoa hotuba ya kila mwaka mbele ya wabunge wa umoja huo iliyogusia orodha pana ya masuala muhimu kwenye kanda hiyo.

https://p.dw.com/p/4WHLN
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, akiwahutubia wabunge wa Ulaya mjini Strasbourg.Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ambacho ni chombo kinachosimamia shughuli za kila siku za umoja huo ameitumia hotuba yake mbele ya wabunge mjini Strasbourg kutoa taswira ya jinsi kanda hiyo inavyoyashughulikia masuala chungunzima ya kipaumbele.

Tangu mzozo wa Ukraine, hali ya uchumi kwenye kanda ya sarafu ya Euro, ushindani wa kibiashara na China na juhudi za kupunguza utoaji wa gesi ya Kaboni.

Kubwa kuliko yote ni vita nchini Ukraine, ambapo Von der Leyen amerejea msimamo wa kanda ya Ulaya wa kuendelea kuisaidia nchi hiyo bila kuchoka katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Pia amegusia mafanikio yaliyopigwa na serikali mjini Kyiv kuelekea azma ya taifa hilo kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Von der Leyen ataka mchakato wa kukaribisha wanachama wapya uwe wa haraka

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen akitoa hotuba yake mbele ya Bunge la Umoja wa Ulaya.Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Amewaambia wabunge wa umoja huo kuwa hatma ya Ukraine imo ndani ya Umoja wa Ulaya na amewarai watunga sheria kuunga mkono uwezekano wa kuharakisha taratibu za kuyakaribisha mataifa mengine ndani ya kanda hiyo bila vizingiti visivyo na kikomo.

Ukraine tayari ilipewa hadhi ya kuwa miongoni mwa mataifa yanayosubiri kujiunga na Umoja wa Ulaya mwezi Juni mwaka jana.

Hata hivyo suala la kupewa rasmi uachama kamili huchukua muda mrefu na wakati mwingine hata kipindi cha muongo mzima na jambo hilo haliwafurahishi viongozi mjini Kyiv.

Ingawa hadi sasa bado hakuna ahadi iliyotolewa ya kuharakisha mchakato wa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya, von der Leyen ametangaza kuendelea kutoa hadhi maalum kwa raia wa Ukraine waliokimbia vita na kuingia kwenye mataifa ya kanda hiyo.

Amesema hawatalazimika kuomba hifadhi na watabakia kwenye nchi walizokimbilia kwa kadri itakavyohitajika.

Umoja wa Ulaya kuchunguza ruzuku ya China kwa waundaji magari ya umeme 

Magari ya China
Magari ya China Picha: HPIC/dpa/picture alliance

Suala jingine lililojitokeza ni tangazo la Von der Leyen kufungua uchunguzi juu ya ruzuku inayotolewa na China kwa makampuni yake yanayounda magari ya umeme.

Von der Leyen amesema mkakati huo wa Beijing unatishia uzani sawa wa ushindani kibiashara kwa kuyafanya magari kutoka China kuwa ya bei nafuu kuliko yale yanayoundwa barani Ulaya.

"Hivi sasa soko la dunia limesheheni magari ya umeme ya bei ya kutupa kutoka China. Na bei yao isiyo halisi inatokana na ruzuku kubwa inayotolewa na serikali. Huko ni kuvuruga soko letu. Na kwa kuwa hatubali mwenendo huo ndani ya soko letu wenyewe, hatukubali vilevile tabia hiyo kutoka nje" amesema Von der Leyen.

Malengo ya nishati, mkakati mpya wa Afrika na hali ya uchumi 

Ama kuhusu lengo la kuachana na nishati chafuzi kwa mazingira, Von der Leyen amewaambia wabunge kuwa Umoja wa Ulaya utatangaza msaada wa kifedha kuyasaidia makampuni yanayofua nishati kwa kutumia upepo.

Tabini za kufua umeme kwa upepo kaskazini mwa Ujerumani
Umoja wa Ulaya unataka kuongeza uzalishaji nishati kwa kutumia upepo Picha: Christian Charisius/Pool/REUTERS

Mataifa ya kanda hiyo yanataka ifikapo mwaka 2030 nishati yote inayotumika iwe imezalishwa kwa vyanzo jadidifu.

Von der Leyen ambaye anatarajiwa kuwania muhula wa pili baada ya uchaguzi wa bunge la Ulaya hapo mwezi Juni mwakani, amezungumzia pia dhamira yake ya kutanua ushirikiano na Afrika.

Anataka Umoja wa Ulaya ubadili mtizamo wake kuelekea bara hilo katika wakati mataifa kama Urusi yanatanua mbawa zake barani humo na mapinduzi ya kijeshi yanatishia uthabiti.

Kuhusu hali ya uchumi kwenye kanda ya sarafu ya Euro, von der Leyen amesema anaridhishwa na mikakati ya Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya katika kupunguza mfumuko wa bei kuelekea lengo la asimilia 2 pekee.