Vuguvugu la Azadi lapania kuipundua serikali ya Pakistan
1 Novemba 2019Shule zimefungwa kwa siku ya pili mfululiizo na msongamano wa magari ukivuruga shughuli za mji huo huku wanajeshi 17,000 wakisambazwa kulinda amani.
Licha ya vizuwizi katika baadhi ya njia kuu waandamanaji waliojazana ndani ya mamia ya magari na mabasi wakiongozwa na Maulana Fazul Rehman mkuu wa chama cha Kiislam cha Jamiat-Ulema-e-Islam wamejipenyeza mjini Islamabad alfajiri wakisubiri amri kutoka kwa viongozi wao kabla ya sala ya Ijumaa.
Rehman ameongozana na vuguvugu hilo wanaloliita " Vuguvugu la Azadi" Au Vuguvugu la Uhuru kutoka mji wa kusini wa Karachi tangu jumapili iliyopita na kuzunguka masafa ya kilomita 2000 hadi kuwasili mji mkuu Islamabad saa sita za usiku, alkhamisi.
Makundi mengine ya upinzani likiwemo lile la rais wa zamani Asif Ali Zardari na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif nayo pia yamejiunga na maandamano hayo na kuzidi kumtia kishindo waziri mkuu Imran Khan.
Waandamanaji wanasema uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa wa hadaa
Rehman, shekhe wa miaka 66 anaetokea katika Chuo cha mafunzo ya kiidini- ya madhehebu ya Sunni cha Deobandi chenye ushawishi mkubwa anamtaka Imran Khan ajiuzulu au akabiliane na wimbi la maandamano la malaki ya wafuasi wake. "Tunakwenda Islamabad kuipindua serikali haramu" alisema Rehman alipowasili karibu na mji mkuu Islamabad.
Waandalizi wa maandamano hayo hawakuwaruhusu wanawake kushiriki na kuzusha lawama katika mitandao ya kijamii.
Vyama vya upinzani vinasema uchaguzi wa mwaka 2018 uliomleta madarakani Khan ulifanyika kutokana na ushawishi wa jeshi na matokeo yake yalikuwa ya hadaa yakilenga kuileta madarakani serikali wanajeshi waliokuwa wanaitaka.
Wanajeshi waliitawala Pakistan kwa takriban nusu ya muda wote tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947.
"Tumetoka ili kushindana na serikali inayotumwa na wanajeshi" msemaji wa Rehman, Ghafoor Haider amesema.
Waziri mkuu Imran Khan anakataa kujiuzulu licha ya malalamiko kuhusu ughali wa maisha.