Vuta nikuvute katika uchaguzi Lower Saxony
21 Januari 2013Hakuna mtafiti wa masuala ya uchaguzi anayekumbuka kutokea kwa ushindi finyu namna hii kama ulivyokuwa katika jimbo la Lower Saxony. Hadi Jumapili usiku haikufahamika bayana iwapo chama cha Christian Democratic Union (CDU) na Waliberali wa Free Democrats (FDP) watabakia madarakani au kung'olewa na muungano wa chama cha Social Democratic (SPD) na kile cha Kijani "Die Grünen". Uchaguzi huu ni mwanzo wa kusisimua katika mwaka huu wa uchaguzi ambapo Kansela Angela Merkel atagombea kipindi cha tatu cha uongozi.
Kwa mpinzani mkuu wa Merkel, Peer Steinbrück wa SPD, uchaguzi wa Lower Saxony ni msaada kwa safari yake ya kumwondoa Merkel madarakani. Chama chake kimepata kura nyingi zaidi ikilinganishwa na uchaguzi uliopita katika jimbo hilo. "Hii inamaanisha kwamba kubadili chama tawala na kupata serikali mpya ni jambo linalowezekana," alisema Steinbrück. Mwanasiasa huyo amekiri kuwa wakati mwingine ameshindwa kukisaidia chama chake kwani mara nyingi amekaririwa akitoa kauli zilizowakera wapiga kura na kuzua mijadala mikubwa. Jambo hilo lilipelekea kuzuka kwa tetesi juu ya kubadilishwa kwa mgombea wa ukansela katika chama cha SPD. Lakini baada ya ushindi katika jimbo la Lower Saxony ni wazi kwamba Steinbrück atabakia kuwa mgombea.
Wapiga kura wa CDU wawasaidia Waliberali
Chama cha Steinbrück kinatarajia kuunda serikali ya muungano na chama cha Kijani iwapo vyama hivyo vitapata wingi wa kura. Hivi sasa maoni ya wapiga kura yanaonyesha kwamba Kijani kitapata kura nyingi zaidi ya zile za uchaguzi mkuu uliopita. Hata katika uchaguzi wa Lower Saxony, asilimia 14 ya wapiga kura walichagua kijani na hivyo kukipa chama hicho matokeo mazuri kuliko miaka ya nyuma.
Tangu kabla ya uchaguzi, Kansela Angela Merkel alikuwa amejiandaa kwa uwezekano wa mbunge wa Niedersachsen, David McAllister wa CDU, kung'olewa madarakani. Maoni ya wapiga kura yalitabiri kwamba mshirika wa CDU, FDP, atapata chini ya asilimia 5 na hivyo kushindwa kuingia kwenye bunge la Lower Saxony. CDU ilianzisha mpango wa kukiokoa chama cha FDP kwa kuwashauri wafuasi wake kupiga kura ya kwanza kwa mgombea wa CDU na kura ya pili kwa FDP. Kwa kawaida, mtu anakuwa na kura mbili ambapo katika kura ya kwanza anamchagua mgombea na katika kura ya pili anachagua chama anachokipendelea. Kwa namna hiyo FDP iliweza kupata asilimia 9.9 ya kura na hivyo kuwa juu ya kiwango kilichotabiriwa.
Hatma ya chama cha Maharamia "Die Piraten" haijulikani
Chama cha mrengo wa kushoto "Die Linken" kimeambulia asilimia 3.1 tu ya kura na hivyo kulazimika kutoka kwenye bunge la Lower Saxony. Katika uchaguzi mkuu uliopita, Die Linken waliwashangaza wengi kwa kupata asilimia 12 ya kura. Lakini kwenye chaguzi zilizopita katika majimbo ya Northrhine Westphalia na Schleswig-Holstein, Die Linken walipoteza pia viti vyao bungeni kwa kupata kura chache sana. Chama hicho kiliundwa mwaka 2005 na kilitokana na wanachama wa SPD waliokuwa na mtazamo wa kushoto zaidi. Kiongozi wake alikuwa mwanasiasa Oskar Lafontaine. Die Linken walipendwa zaidi katika majimbo ya iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki. Inatarajiwa kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba, Die Linken kwa mara nyingine watapata viti bungeni kwa sababu ya wafuasi wengi Ujerumani ya Mashariki.
Chama cha "Die Piraten", kinachopigania uhuru zaidi katika mtandao wa internet, nacho kimeshindwa kuingia katika bunge la Lower Saxony kwa kupata asilimia 2.1 tu ya kura na hivyo kuwa chini ya kiwango cha asilimia 5 kinachohitajika. Katika siku za nyuma chama hicho kiligonga vichwa vya habari kwa taarifa za mgawanyiko ndani ya chama. Utafiti wa wapiga kura kwa uchaguzi mkuu ujao unatabiri kwamba Die Piraten hawatapata zaidi ya asilimia 3 ya kura na hivyo hawatakuwa na wawakilishi katika bunge la Ujerumani.
Mwandishi: Bernd Gräßler
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Khelef