Vyama tawala Kongo vya pata wingi wa viti bungeni
14 Januari 2024Chama cha UDPS cha Rais wa Kongo Felix Tshisekedi kimeshinda asilimia 12 ya viti vya bunge katika uchaguzi wa Desemba, na kukiweka chama hicho mbele ya vyama vingine 44 vilivyopata kiti kimoja au zaidi katika jumla ya viti 500 kwenye bunge la nchi hiyo.
Kwenye matokeo ya uchaguzi yaliotangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini Kongo, CENI, chama cha UDPS kimepata viti 66 katika uchaguzi uliomalizika.
Chama hicho kilipata viti 35 vya bunge kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2018. Rais Tshisekedi pamoja na vyama washirika watakuwa na wingi wa viti bungeni.
Ushindi wa vuguvugu la ''Union Sacrée''
Matokeo ya muda yaliyotangazwa na Tume ya uchaguzi yameonyesha kuwa vyama vinavyoongozwa na baadhi ya Washirika wa Tshisekedi akiwemo Spika wa Seneti Modeste Bahati Lukwebo, Waziri wa Ulinzi Jean Pierre Bemba na Waziri wa Uchumi Vital Kamerhe vilishinda zaidi ya viti 80 vya bunge.
Matokeo ya kura ya ubunge yametolewa baada ya Mahakama ya Katiba kuthibitisha kuchaguliwa Rais Tshisekedi katika uchaguzi ambao ulighubikwa na tuhuma za udanganyifu, upungufu wa vifaa na usumbufu.
Vyama vya upinzani na waangalizi huru wa uchaguzi wamelezea wasiwasi wao kuhusu uwazi wa uchaguzi huo, wakitoa mfano wa machafuko, masharti ya upigaji kura na mchakato wa kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Kasoro za uchaguzi za fumbiwa macho ?
Serikali kadhaa za nchi za magharibi zimempongeza Tshisekedi kwa kuchaguliwa, na anatarjiwa kuapishwa ili kuongoza muhula mwingine wa miaka mitano kama kiongozi wa nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya muhula wa kwanza uliokumbwa na matatizo ya kiuchumi na mgogoro wa kiusalama kwenye mikoa ya mashariki.
Kupingwa kwa matokeo ya uchaguzi kunatishia kuiyumbisha zaidi Kongo, nchi ya tatu kwa uzalishaji wa shaba duniani. Vyama vya upinzani nchini humo vimelaumu mara kwa mara kwamba uchaguzi huo ulijaa visa vya udanganyifu na vimetaka uchaguzi huo urudiwe lakini mapendekezo hayoyametupiliwa mbali na mamlaka.
Msimamo wa Tume ya uchaguzi
Kwa upande wake Tume ya uchaguzi, CENI imesema uchaguzi ulikuwa wa kuaminika, ingawa ilibatilisha matokeo ya wagombea 82 wa nafasi za ubunge kati ya wagombea laki moja kwenye chaguzi zote nne zilizofanyika Desemba 20.