1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Waangalizi wa uchaguzi wanyimwa vibali vya kuingia Venezuela

27 Julai 2024

Mamlaka nchini Panama imesema ndege iliyowabeba marais wanne wa zamani wa mataifa ya Marekani ya Kusini walionuia kwenda Venezuela kama ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa urais, imenyimwa kibali cha kuingia Venezuela.

https://p.dw.com/p/4ioSt
Kombibild Wahl in Venezuela 2024 | Nicolas Maduro und Edmundo Gonzalez Urrutia
Wagombea uras Nicolas Maduro (kushoto) na Edmundo Gonzalez Urrutia (kulia)Picha: Yuri Cortez/AFP/Rances Mattey/Anadolu/picture alliance

Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Panama Javier Martinez-Acha, Venezuela imeamua kuifunga anga yake kwa shirika la ndege la Copa Airlines kwa saa kadhaa.

Venezuela hata hivyo imekanusha madai kwamba imewazuia viongozi hao wa zamani kuingia nchini humo. Mamlaka ya usafiri wa anga ya Venezuela kupitia taarifa imesema anga yake imekuwa wazi na inaruhusu safari za ndege.

Soma pia: Upinzani Venezuela wamsajili mgombea wa uchaguzi wa rais

Rais wa Panama Jose Raul Mulino ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa X kuwa, rais wa zamani wa nchi hiyo Mireya Moscoso, rais wa zamani wa Mexico Vicente Fox, rais wa zamani wa Costa Rica Miguel Ángel Rodríguez na rais wa zamani wa Bolivia Jorge Quiroga walipaswa kuelekea mji mkuu wa Venezuela Caracas lakini wakalazimishwa kusitisha safari zao baada ya ndege yao kunyimwa kibali cha kuingia Venezuela.

Rais wa muda mrefu wa Venezuela Nicolas Maduro anatarajiwa kushinda muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi ambao waangalizi wanaamini hautafanyika kwa njia huru na haki.